METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, October 22, 2018

RC MTAKA ATOA WITO KWA WANANCHI KUJITOKEZA KWA WINGI MAONESHO YA SIDO KITAIFA SIMIYU




Na Stella Kalinga, Simiyu

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ametoa wito kwa wananchi mkoani humo na maeneo mengine nchini kujitokeza kwa wingi kushirikia katika  Maonesho ya Kitaifa ya Viwanda Vidogo (SIDO), yatakayofanyika kuanzia Oktoba 23-28, mwaka huu katika Viwanja vya Nyakabindi Bariadi mkoani humo na kubainisha kuwa Maandalizi yote yamekamilika.

.Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Mtaka amesema Maonesho haya yatafunguliwa rasmi siku ya Jumanne Oktoba 23, 2018 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.

Ameongeza kuwa katika maonesho hayo wajasiriamali, waoneshaji wa teknolojia mbalimbali wamealikwa na kusisitiza kuwa hii ni fursa kwa wananchi wa Mkoa wa Simiyu na mikoa mingine kuona ushindani katika uongezaji wa thamani wa mazao mbalimbali na fursa kwa wajasiriamali kujifunza kutoka kwa wenzao.

“ Nitoe wito kwa wananchi wa mkoa wa Simiyu kujitokeza kushiriki maonesho haya maana hii ni fursa kwao ya kuweza kujielimisha katika maeneo mbalimbali ya teknolojia za viwanda hususani viwanda vidogo, lakini pia wajasiriamali watapata nafasi ya kujifunza kutoka kwa wenzao wa maeneo mengine nchini na nje ya nchi” alisema Mtaka.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Masoko na Uwekezaji wa  Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Shoma Kibende amesema tayari wajasiriamali kutoka mikoa mbalimbali wamethibitisha kushiriki  maonesho hayo na baadhi yao wameanza kuwasili.

“Wajasiriamali zaidi ya 1000 kutoka mikoa yote nchini wanatarajia kushiriki maonesho haya na baadhi yao wameshaanza kuwasili, lakini pia kuna taasisi mbalimbali ambazo ni taasisi shirikishi na SIDO, huduma za kupata ubora hii ni fursa pekee kwa Watanzania” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe amesema zaidi ya wajasiriamali 51 kutoka wilayani humo watashiriki katika kuonesha bidhaa mbalimbali ambazo wametengeneza na kuzalisha kupitia viwanda vidogo.

Naye Meneja wa SIDO Mkoa wa Kagera,Richard Mahela amesema maonesho ya SIDO ambayo ni ya kwanza kufanyika Kitaifa  yatawasaidia wajasiriamali kote nchini kupanua masoko ya bidhaa zao kwa kuwa wameandaa vipeperushi vya bidhaa zao ambavyo  vitasambazwa kwa lengo la kusaidia kuwaunganisha na wanunuzi.

Maonesho ya Viwanda Vidogo (SIDO) Kitaifa ambayo ni ya kwanza kufanyika ngazi ya Kitaifa yatafunguliwa rasmi Jumanne Oktoba 23, 2018 na kuhitimishwa siku ya Jumapili Oktoba 28, 2018 yakiwa na Kauli Mbiu: PAMOJA TUJENGE VIWANDA KUFIKIA UCHUMI WA KATI”.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com