METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, October 11, 2018

HALMASHAURI ZA RUKWA ZATENGA SH.MIL.79 KUNUNUA MBEGU ZA KAHAWA


Zao la kahawa ni miongoni mwa mazao matano ya biashara ambayo serikali ya awamu ya tano imeamua kwa dhati kutilia mkazo uzalishaji wake, kwa mkoa wa Rukwa zao hilo ndio zao ambalo limeonekana kustawi kwenye baadhi ya maeneo na kupelekea halmashauri za mkoa huu kutenga shilingi milioni 79 kwaajili ya kununua mbegu ili kuendeleza zao hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesema kuwa kama mkoa hatuna budi kutilia mkazo uanzishaji na uendelezaji wa zao hili ili wakulima wetu waweze kuwa na zao la biashara na kubainisha kuwa tayari maeneo kwaajili ya kilimo hicho yameshabainishwa ambapo makampuni, taasisi na wakulima wameonyesha nia ya kulima.
“Eneo la kiasi cha ekari 3,195.83 limebainishwa kwa ajili ya kulimwa zao la kahawa. Jumla ya wakulima 2,266 na taasisi 9 zitajihusisha katika uzalishaji wa kahawa. zikiwemo taasisi za Jeshi la Magereza pamoja na Jeshi la Wananchi Tanzania.”Alisema.
Ameyasema hayo katika kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) kilichofanyika mwezi huu wa nane katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa Mkoa ikijumuisha wadau mbalimbali wa maendeleo, Wabunge, Madiwani, Viongozi wa dini na wataalamu wa Halmashauri na sekretarieti ya mkoa.
Aidha, mbunge wa viti maalum Mkoa wa Rukwa Mh. Aida Khenan amesema kuwa kilimo cha kahawa kinahitaji wakulima wenye uwezo wa kifedha ambao katika mkoa wa rukwa wakulima hao hawapo na kusisitiza kuwa wakulima wa mkoa huo wamezoea kilimo cha muda mfupi.
“kahawa inahitaji fedha na muda, wakulima wetu wamezoea kilimo cha muda mfupi, watakaoweza kumudu kahawa ni wale wenye uwezo, masuala ya madawa na kuhudumia hiyo kahawa, wataalamu wetu wafanye utafiti watuambie zao lipi la kibiashara litaleta tija kwa wananchi wetu hasa katika msimu huu wa kilimo,” Alisema.
Mh. Wangabo alieleza kuwa mkoa umejipanga katika kuhamasisha kilimo cha zao la alizeti kama zao la kibiashara kwani hali ya uzalishaji wa zao hilo kwa sasa hairidhishi na hivyo kutoleta tija kwa wakulima.
“Hali ya uzalishaji wa zao la alizeti katika Mkoa umebaki kuwa ni wastani wa gunia  6.5 za kilo 65  kwa ekari sawa na  tani 1.1 kwa hekta. Tija hii ni ndogo sana ukilinganisha na tija iliyofanyiwa utafiti ya gunia 12-16 kwa ekari ambazo ni sawa na zaidi ya tani 2.00 kwa hekta.” Alibainisha.
Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kutilia mkazo uzalishaji wenye tija wa mazao matano ya biashara ambayo ni Korosho, Chai, Kahawa, Tumbaku na Pamba.
IMETOLEWA NA 
OFISI YA MKUU WA MKOA WA RUKWA 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com