METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, September 16, 2018

WANANCHI WILAYANI BARIADI WARIDHIA KUACHIA MAENEO YAO KUPISHA UJENZI WA KIWANJA CHA NDEGE CHA KIMATAIFA SIMIYU


Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ng’arika  Kata ya Sapiwi Septemba 14, 2018 wilayani humo, katika Uzinduzi wa zoezi la uthamini  na upimaji wa maeneo ambayo Kiwanja cha  Ndege cha Kimataifa cha Simiyu kitakapojengwa .
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Ng’arita katika Kata ya Sapiwi Wilaya ya Bariadi, wakinyoosha mikono yao juu kumhakikishia Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. Festo Kiswaga kuonesha utayari wao wa kuachia maeneo yao kupisha Ujenzi wa Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha mkoa  huo, wakati wa Mkutano wa kufungua Zoezi la tathmini na upimaji wa maeneo hayo, Septemba 14, 2018.

Na Stella Kalinga, Simiyu

Wananchi wa Vijiji vya Igegu na  Nga’arita Kata ya Sapiwi wilayani Bariadi  wameridhia kuachia maeneo yao kupisha Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Mkoani Simiyu ambacho kinatarajiwa kujengwa katika eneo la Igegu wilayani .

Wananchi hao wameyasema hayo Septemba 14, 2018 wakati wa uzinduzi wa zoezi la Uthamini na upimaji wa maeneo hayo, ambalo linatarajiwa kumalizika baada ya mwezi mmoja na wiki mbili kuanzia sasa.

Wamesema kuwa wamefurahishwa na hatua ya Serikali kujenga Kiwanja cha Ndege wilayani Bariadi na kwa kuwa ujenzi huo ni suala la maendeleo hawawezi kupinga, huku wakiiomba Serikali kuhakikisha wanalipa fedha za fidia kwa wakati mara tu baada ya kukamilisha zoezi la uthamini na upimaji wa maeneo hayo.

“Kwa kuwa ujenzi wa kiwanja cha ndege ni maendeleo hatuwezi kukataa kutoa maeneo yetu, tumekubali kutoa maeneo ila ombi letu kwa Serikali tunaomba tulipwe fidia ya maeneo yetu kwa wakati na tulipwe kwa haki” alisema Ndaturu Malemi mkazi wa Kijiji cha Igegu.

“Tumekubali kutoa maeneo yetu Uwanja wa Ndege ujengwe, ushauri wangu tu ni kwamba kwa kuwa tunaelekea msimu wa kuandaa mashamba baada ya tathmini tunaomba tuliokuwa na maeneo hapa tuambiwe mapema kama ujenzi utaanza au  tunaweza kuendelea na shughuli za kilimo”alisema Mahembe Mayumba mkazi wa Kijiji cha Igegu

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga amewataka Wataalam wa Ardhi watakaohusika na zoezi la uthamini  na upimaji wa eneo litakojengwa Kiwanja hicho cha Ndege kufanya zoezi hilo kwa kufuata haki na sheria za nchi.

“Nimewaagiza wataalam watakaohusika kufanya zoezi la tathmini na kulipa fidia kwa kumuogopa Mungu, watende haki, kila ambacho mwananchi anapaswa kufidiwa wahakikishe kinafidiwa kwa mujibu wa sheria; tumekubaliana wataalam watavaa vitambulisho ili watambuliwe na ikitokea mtu akihujumu zoezi hili iwe rahisi kumfahamu na kuchukua hatua” alisema Kiswaga.

Akizungumzia suala la taarifa ya uthamini  kutolewa mapema kwa wananchi, Kiswaga amesema kuwa zoezi hilo litafanyika kwa muda wa mwezi mmoja na wiki mbili na baada ya hapo wenye maeneo watapewa taarifa.

Meneja wa Kiwanja cha Ndege Shinyanga Bi.Beaster Dotto  Madale amesema Ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa utawasaidia wananchi kupata usafiri wa anga ambao ni wa haraka, uhakika na salama, huku akisisitiza kuwa kiwanja hicho kitakapoanza kujengwa wananchi hususani vijana watapata ajira kwenye kazi za ujenzi na wanawake watajiajiri katika kazi za kupika na kuuza vyakula

Naye Afisa Ardhi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Bi.  Bi. Cecilia Mwing’uri   amesema Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege Nchini (TAA) imeshatoa fedha kwa ajili ya tathmini, uthamini na upimaji wa maeneo Kiwanja kitakapojengwa na mara baada ya zoezi hilo kukamilika wananchi wanaohusika watalipwa fidia.

Bi.Cecilia amewahakikishia wananchi wa Vijiji vya Igegu na Ng’arita kuwa watalipwa fedha zao zote mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uhakiki , kwa kuwa  Mamlaka ya Viwanja Vya Ndege Nchini (TAA) imetenga fedha hizo kwa ajili ya fidia ya Kiwanja cha Ndege cha Simiyu.

Kwa mujibu wa Meneja wa Kiwanja cha Ndege Shinyanga Bi.Beaster Dotto  Madale Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa Mkoani Simiyu kitakapokamilika kitakuwa ni miongoni mwa Viwanja vikubwa hapa nchini ambavyo  vina uwezo wa kupokea ndege kubwa.

MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com