METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, July 6, 2018

DKT ANGELINE MABULA AHITIMISHA ZOEZI LA UTOAJI BURE HUDUMA ZA AFYA KITUO CHA AFYA BUZURUGA

Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula leo amezuru kituo cha afya Buzuruga kukagua zoezi la utoaji wa huduma za afya kwa wananchi linavyoendeshwa kituo hapo pamoja na kuhitimisha zoezi la upimaji virusi vya ukimwi kwa hiari na utoaji bure wa matibabu lililokuwa likiendeshwa na wataalamu wa afya kutoka manispaa ya Ilemela kwa kushirikiana na wanafunzi wa chuo cha Calfonia kilichopo nchini Marekani.

Akizungumza wakati wa uhitimishaji wa zoezi hilo Dkt Angeline Mabula mbali na kushukuru timu ya wataalamu kutoka nchini Marekani kwa kukubali kushirikiana na jimbo lake katika kutoa huduma za afya kwa wananchi wake, Ametaja faida mbalimbali zilizopatikana kupitia ugeni huo ikiwemo upatikanaji wa vifaa tiba na ushirikiano endelevu katika upatikanaji wa huduma za uhakika za afya kwa kipindi chengine.

'... Tunashukuru zoezi limekwenda vizuri pia tunawakaribisha wengine watakaoweza kujitokeza tushirikiane kuendesha zoezi la namna hii, Pamoja na kwamba zoezi litaendelea lakini tunashukuru tumepata vifaa  vitakavyotumiwa na madaktari wetu ...' Alisema

Aidha Mhe Mabula ametaja changamoto mbalimbali zilizokabili zoezi  hilo ikiwemo tofauti ya lugha inayozungumzwa na mtoa huduma na mfata huduma sambamba na siku chache za uendeshwaji wa zoezi ukilinganisha na uhitaji huku akiwaahidi wananchi wa Jimbo lake kuwa wavumilivu na kujitokeza pindi itakapoanza awamu nyengine ya uendeshwaji wa zoezi kama hilo litakaloanza hivi karibuni kwa kushirikiana na shirika la ICAP nalo likitokea nchini Marekani.

Kwa upande wake Mwanafunzi kutoka chuo cha Calfonia nchini Marekani aliyekuwa akishiriki uendeshaji wa zoezi la utoaji huduma za  upimaji wa hiari wa ugonjwa wa Ukimwi Justine Maher amemshukuru Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt Angeline Mabula na wataalamu wa manispaa ya Ilemela kwa ushirikiano waliouonesha wakati wa zoezi huku akiahidi kurudi tena na wenzake kuendelea na zoezi hilo sanjari na kuongeza idadi ya vituo kwa kuhudumia vituo vyote vya afya vinavyopatikana ndani ya jimbo hilo.

Akihitimisha mkazi wa Buzuruga aliyenufaika na uendeshwaji wa huduma iliyokuwa ikitolewa kituoni hapo Bi Helena Kiyeri amempongeza Mbunge wa Jimbo la Ilemela kwa kuwatembelea kituoni hapo kujionea zoezi la utoaji wa huduma za afya linavyoendeshwa pamoja na juhudi zake za kushirikiana na wadau mbali mbali katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo ndani ya jimbo lake huku akiwaomba viongozi wengine kuiga mfano huo.

Aidha zoezi la utoaji wa huduma za afya liloendeshwa kituo cha afya cha Buzuruga lilichukua muda wa wiki moja na kuwafikia wananchi zaidi ya mia saba huku kati ya wananchi mia sita sabini na nne waliopimwa mpaka kufikia jana wananchi mia moja kumi na moja walionekana wana tatizo na wananchi kumi na moja kuonekana uhitaji wa kupatiwa rufaa  kwenda hospitali ya rufaa ya sokou toure kwa matibabu zaidi  waliotoka maeneo mbalimbali ya jimbo la Ilemela na wilaya zilizo jirani na jimbo hilo.

' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga'

Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
06.07.2018

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com