Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko
Na George Binagi, Ruvuma
Naibu Waziri
wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko ameutaka uongozi wa kampuni ya TANCOAL inayochimba
madini ya makaa ya mawe katika machimbo ya Ngaka yaliyopo Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma kufanya kazi kwa kufuata sheria na kuacha mara moja ujanja ujanja
wa kukwepa kodi.
Aidha
Mhe Biteko ametoa muda wa mwezi mmoja kwa kampuni hiyo kuwa imelipa serikalini
malimbikizo yote ya mrabaha ambayo yanafikia hadi bilioni mbili kabla haijaandikiwa Samansi ya makosa inayoweza kusababisha kunyang’anywa leseni ya uchimbaji.
Mhe Biteko
aliyasema hayo jana Julai 17, 2018 alipofanya ziara katika mgodi huo na kukuta uongozi wa kampuni ya TANCOAL unalipa mrabaha serikalini kwa bei ya kununulia
madini mgodini badala ya bei ya mwisho ya kuuzia madini baada ya kusafirishwa.
Alisema kifungu
cha 87 cha sheria ya madini, kifungu kidogo cha sita kinaeleza wazi kwamba kodi
ya madini itatathiminiwa kwa bei ya mwisho ya kuuzia huku kifungu cha 18
kikitoa mamlaka kwa mtu yeyote anayesafirisha madini kuwa na leseni ya kuchimba
madini ama leseni ya Wakala lakini kampuni ya TANCOAL inatoa leseni yake kwa
wateja ili kusafirishia madini hayo mwanya ambao unatumika kukwepa kodi.
Mhe Biteko
alisema kitendo cha wanunuaji wa madini ya makaa ya mawe kutumia leseni ya
TANCOAL kusafirishia madini hayo ni kinyume cha sheria ambapo wao wanakwenda kuyauza
kwa bei ya juu mara tatu zaidi huku TANCOAL ikilipwa mrabaha wa dola 44 kwa
tani moja.
Awali Mkuu
wa Mkoa Ruvuma Mhe Christina Mndeme alisema watanzania wanapaswa kuwa wazalendo
na kumuunga mkono Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika kusimamia rasilimali za Taifa
ikiwemo madini huku akitoa rai kwa taasisi ya NDC (National Development
Corporation) kuweka wawakilishi wake katika eneo la mgodi wa Ngaka pamoja na
eneo la mizani ili kufuatilia taarifa za uuzaji wa madini ya makaa ya mawe.
Kaimu Meneja
wa kampuni ya TANCOAL, Edward Mwanga alisema wateja wao ikiwemo kampuni ya Lake
Ciment, Dangote Ciment pamoja na Tanga Ciment hawana leseni ya kusafirishia
madini ndiyo maana kampuni ya TANCOLA hutoa leseni yake kwa kampuni hizo.
Mkuu wa Mkoa Ruvuma Mhe Christina Mndeme akizungumza kwenye kikao baina ya Naibu Waziri na uongozi wa kampuni ya TANCOAL.
Kaimu Meneja wa kampuni ya TANCOAL, Edward Mwanga akizungumza kwenye kikao hicho
Naibu Waziri wa Madini Mhe.Doto Biteko akikagua eneo la Bandari Kavu lililopo Kijiji cha Amani Makolo wilayani Mbinga
Naibu Waziri wa Madini Mhe.Doto Biteko akikagua eneo la machimbo ya makaa ya mawe Ngaka wilayani Mbinga
Machimbo ya Ngaka yanapochimbwa madini ya Makaa ya Mawe ambayo hutumika kwa ajili ya uzalishaji wa umeme wa viwandani
0 comments:
Post a Comment