METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, June 15, 2018

Kongwa Wafanya ziara Mkoani Simiyu Kutembelea Miradi ya Vijana ili Kujifunza

Viongozi kutoka Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Deo Ndejembi pamoja na baadhi ya viongozi wa vikundi vya vijana wilayani humo wamefanya ziara Mkoani Simiyu ili kujifunza namna vikundi vya vijana vinavyotekeleza miradi yake.
Timu hiyo imefanya ziara ya siku mbili hadi Juni 08, 2018  katika miradi inayotekelezwa na vijana kwa kushirikiana na Halmashauri ambayo ni Kiwanda cha Chaki,  Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi wilayani Maswa na Mradi wa kiwanda cha kusindika maziwa wilayani Meatu.
Mkuu wa wilaya ya Kongwa amesema wameamua kuja Simiyu kwa kuwa vikundi vyake vimeonekana vikifanya vizuri katika miradi yake, hivyo wamewaleta vijana wao ili wapate uzoefu na ari itawasukuma kubuni miradi yao na kujua namna bora ya kuiendesha.
"Tumeona tuje tujifunze kutoka Simiyu maana mkoa wa Simiyu umeonesha mfano wa namna vikundi vya vijana vinavyotakiwa kutekeleza miradi yake, tumeona kwenye vyombo vya habari na kwingineko mkipata sifa nyingi kutokana na miradi yenu kuonesha matokeo, nia yetu vijana waje waone wajifunze wapate hasira ya kufanya kitu cha kwao" alisema Ndejembi.
Ndejembi amesema ni matamanio yake kuona vijana wa Kongwa wanaanzisha miradi ya viwanda kama ilivyo kwa Maswa na Meatu kwa kuwa wilaya hiyo ndiyo inayofanya vizuri katika kilimo na ufugaji Mkoani Dodoma ambapo uzalishaji wa malighafi ya viwanda hivyo uko vizuri pia.
Ameongeza kuwa baada ya ziara hiyo vijana wake wamejifunza hivyo watakapofika wilayani Kongwa wataenda kufanya miradi ambayo itakuwa ya mfano na endelevu kwa kuwa tayari wana wafadhili waliokubali kutoa fedha kwa ajili ya kuanzisha miradi hiyo.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Dkt. Omary Nkullo amesema Halmashauri itahakikisha inatoa fedha kuwawezesha vijana kutekeleza miradi yao na itawasimamia ili waweze kufikia ndoto zao.
Akizungumza kwa niaba ya vijana kutoka Kongwa waliofika Simiyu kujifunza, Bw. Zamoyoni George amesema kuja kwao Simiyu hakutakuwa bure bali itakuwa chachu ya kuanzisha miradi endelevu na yenye tija ambayo hata vijana wa Simiyu wataenda kujifunza kwao.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe amewapongeza wilaya ya Kongwa kuona umuhimu wa kujifunza na kuwashauri kuwa fedha wakazozitoa kwa vijana kupitia asilimia tano za mapato ya Halmashauri, zielekezwe kutekeleza miradi ambayo italeta tija na kurejesha fedha za Halmashauri kwa wakati.
Aidha, Dkt. Shekalaghe amesema  Maswa itaendelea kuboresha ubora na biashara ya chaki (MASWA CHALKS)  na kuomba Wilaya ya Kongwa kuanza kununua Chaki za Maswa na kutumia katika shule zake, huku akisisitiza timu hiyo ya Kongwa pia kwenda kutangaza bidhaa za Ngozi zinazozalishwa Kijiji cha Senani wilayani humo.
Mkurugenzi wa Wilaya ya Meatu, Bw. Fabian Manoza akitoa maelezo juu ya  kiwanda cha maziwa amesema Halmashauri ina mpango wa kukipanua kiwanda hicho na Benki ya Maendeleo ya Kilimo imekubali kutoa mkopo wa shilingi bilioni 6 kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda hicho na kuboresha teknolojia ya uzalishaji ili kifikie uwezo wa kuzalisha lita 15,000 kwa siku kutoka lita 800 za sasa.
Mkoa wa Simiyu ni mkoa uliojipambanua kama mkoa wa Viwanda kupitia Falsafa yake ya “Wilaya Moja Bidhaa Moja Kiwanda Kimoja” ambapo umedhamiria kujenga uchumi wa viwanda kwa kutumia malighafi yake inapatikana hapa nchini.
MWISHO
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com