METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, May 23, 2018

TANZANIA INAHITAJI WAWEKEZAJI – WAZIRI MKUU


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania bado inahitaji wawekezaji na kupitia kwenye uwekezaji, inapata fursa ya mitaji na teknolojia za kisasa.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Mei 23, 2018) wakati akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini Canada, Bw. Alfayo Kidata ambaye alifika kumuaga kwenye makazi yake jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu amemtaka Balozi Kidata atumie fursa ya uwepo wake nchini Canada kuangalia namna ya kuisadia nchi kuimarisha sekta za kilimo, madini na utalii.

“Tukiimarisha sekta hizi, uchumi ndani ya nchi unakua lakini pia tunategemea kutumia nchi rafiki kukuza uchumi wetu wa ndani kwa maana ya kukuza mitaji na kupata teknolojia za kisasa,” amesema.

“Ukienda huko mkakati wako mkubwa uwe ni kuzingatia mpango wa Taifa wa maendeleo wa miaka mitano lakini zaidi mkakati wetu wa kukuza uchumi wa viwanda,” amesisitiza.

Amemtaka Balozi huyo akasimamie pia suala la upatikanaji wa masoko kwa ajili ya mazao yanayozalishwa nchini ili wafanyabiashara na wakulima wa Tanzania waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi.

“Hapa nyumbani tuna mazao matano ambayo tumeazimia kuyafufua lakini masoko ya ndani hayatoshi, kwa hiyo kazi yako mojawapo ukiwa huko ni kututafutia masoko,” amesema.

Waziri Mkuu amemweleza Balozi Kidata azingatie pia suala zima la kuongeza idadi ya watalii. “Tunataka ukasaidie kutangaza nchi yetu ili watalii waje kuona vivutio vyetu. Tunataka kuongeza idadi ya watalii kutoka milioni mbili ya sasa hadi kufikia milioni tano ifikapo mwaka 2020,” amesema.

Alimtaka Balozi huyo akafuatiilie pia fursa za masomo kwa ajili ya Watanzania wanaotaka kusoma Canada na Cuba. “Nilipoongea na Makamu wa Rais wa Cuba, aliahidi kuongeza idadi ya Watanzania wanaotaka kusomea udaktari. Kwa hiyo, ukifika itabidi ufuatilie ahadi hiyo,” ameongeza.



Waziri Mkuu pia alimsisitizia Balozi Kidata akifika huko awatambue na kuwaunganisha Watanzania waishio Canada na awahamasishe wafanye kazi ili waweze kuwekeza nyumbani.

Kwa upande wake, akizungumza baada ya kuagana na Waziri Mkuu, Balozi Kidata alisema atahakikisha anayafanyia kazi maelekezo yote aliyopewa na Waziri Mkuu.

Alisema anatambua kwamba Canada ina idadi ya watu zaidi ya milioni 40 na atafanya juhudi zaidi za kuitangaza Tanzania ili waje kuona vivutio vilivyopo nchini. Pia atafuatilia fursa za mafunzo kwa wanafunzi wa Kitanzania.

“Kwenye suala la uchumi wa viwanda, tunahitaji kuwa na uzalishaji wa mazao ya kutosha. Kwa hiyo tunahitaji kuwana kilimo cha uhakika na cha muda wote kuliko. Tunahitaji kupata utaalamu na mitaji kwa ajili ya mashamba ya umwagiliaji,” alisema.

Alisema kuwepo kwa kilimo cha umwagiliaji, kutasaidia kuwe na uhakika wa upatikanaji wa malighafi zitazakotumika kwenye viwanda.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, MEI 23, 2018.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com