Na. Stella Kalinga, Simiyu
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema dhamira ya
Kanda mpya ya Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Nane Nane ya Ziwa
Mashariki inayojumuisha mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga ni kuwa na Uwanja wa
Nanenane utakaofanya Maonesho ya Kilimo Biashara.
Mtaka amesema hayo
wakati akifungua kikao cha Maandalizi ya Maonesho ya Nanenane ya
Kanda ya Ziwa Mashariki yatakayofanyika katika viwanja vya Nyakabindi
kilichowakutanisha Wakuu wa Mikoa mitatu ,Wakuu wa Wilaya na
Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri na Sekretarieti za
Mikoa hiyo, ambacho kilifanyika mjini Bariadi.
Amesema pamoja na
kufanya maonesho ya Kilimo Nanenane ambayo huwa yanafanyika kuanzia Agosti Mosi
hadi Agosti 08 kila mwaka, kutafanyika Maonesho mengine mara nne kwa
mwaka pamoja na matukio mengine yatakayofanyika katika uwanja huo ili kuwe na
tija kwa Halmashauri kuwekeza fedha katika uwanja huo.
“Haiwezekani
Halmashauri zetu zikawekeza katika uwanja wa NaneNane halafu uwanja uwe
unatumika kila tarehe 01 hadi 08 mwezi wa nane kila mwaka tu, ni
lazima tuwe na viwanja ambavyo vitafanya maonesho ya kilimo biashara
lakini eneo lile ukiacha maonesho haya ya NaneNane tutafanya maonesho mara nne
kwa mwaka” alisema.
Ameongeza kuwa ili
kuendana na hali ilivyo sasa ni vema Halmashauri zikakubaliana kujenga jengo la
maonesho (exhibition hall) na kuwa na maeneo ya nje kwa ajili ya vipando
na mifugo kama ilivyopendekezwa katika vikao vya awali, badala ya
kutumia vibanda na mahema kama ilivyozoeleka, ili kuifanya Nane Nane ya Kanda
Mpya ya Ziwa Mashariki kuwa ya tofauti.
Katika kikao hicho, Halmashauri 21 za Mikoa ya Mara, Shinyanga
na Simiyu zimeagizwa kuwasilisha mchango wa kiasi cha shilingi
milioni 20 ndani ya siku sabakwa ajili ya malipo
ya awali ya ujenzi wa jengo la maonesho, huku Mkuu wa Mkoa wa Mara,
Mhe. Adam Malima akiwataka Wakurugenzi kutelekeleza agizo hilo.
“.....tumekubaliana kuwa kila Halmashauri itatoa shilingi
milioni 20 na hili si jambo la masihara, .....ndani ya siku saba tukitoka hapa
kila Mkurugenzi atakuja na hundi yake ya shilingi milioni 20, ili itakapofika
Juni Mosi haya mambo yakamilike” alisema Malima.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhe. Glorius Luoga ametoa wito
kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote katika mikoa hiyo kuwa wabunifu katika
kuhakikisha fedha za kuwezesha ujenzi wa jengo hilo linalotarajiwa kugharimu
jumla ya shilingi bilioni 2.1 zinapatikana.
Hivi karibuni Wizara
ya kilimo imetangaza Kanda Mpya ya Maonesho ya Nanenane ijulikanayo kama Kanda
ya Ziwa Mashariki, ambayo inajumuisha mikoa ya Simiyu, Mara na Shinyanga na
Uwanja utakaotumika kwa ajili ya Maonesho hayo uko Eneo la Nyakabindi Mjini
Bariadi Mkoani Simiyu, ambapo mwaka 2018 Kanda hiyo itakuwa mwenyeji wa
maonesho hayo kitaifa.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment