Na
Munir Shemweta, Morogoro
Waziri wa Katiba na
Sheria Profesa Palamagamba Kabudi amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha
watumishi katika mipango ya uendeshaji Taasisi kwa kuwa suala hilo lipo
kisheria.
Aidha, alisema kwa
miaka yote Serikali imekuwa ikisisitiza Taasisi kujenga na kutekeleza utaratibu
wa kushirikisha watumishi na hali hiyo inatokana na ukweli kuwa palipo na
watumishi wengi pana mawazo mengi.
Profesa Kabudi alisema
hayo mwishoni mwa wiki wakati akifungua mkutano wa kumi na tatu wa Baraza la
Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania uliofanyika katika ukumbi wa
Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) mkoani Morogoro.
‘’Ushirikishwaji
watumishi kwenye mipango ya uendeshaji ofisi unasaidia kupata mawazo mengi na
mapya yanayoweza kurahisisha uendeshaji wa ofisi na kutoa fursa ya kusikiliza
kero na changamoto kwenye uendeshaji wa Taasisi na kushirikiana katika kutafuta
ufumbuzi’’ alisema profesa Kabudi.
Aliongeza kuwa, kwa
kushirikiana na watumishi ni dhahiri wanapata morari wa kushiriki kikamilifu
kwenye utekelezaji wa mipango ya taasisi ambayo wao wenyewe walishiriki
kuiandaa.
Waziri huyo wa Katiba
na Sheria alisema, ushirikishwaji unafanywa kupitia baraza la wafanyakazi kwa kuwa baraza ni chombo kinachowashirikisha
wafanyakazi katika kupanga , kusimamia
na kutekeleza mipango mbalimbali
inayohusu shughuli za kazi za Taasisi kama zilivyoainishwa katika sheria za
nchi.
Kwa mujibu wa Profesa
Kabudi, Mabaraza hutoa fursa kwa wafanyakazi kushiriki katika maamuzi
mbalimbali na kuboresha uhusiano baina ya wafanyakazi na uongozi pamoja na mazingira ya utendaji hasa mahala pa kazi hivyo baraza ni chombo
cha kuimarisha na kuboresha demokrasia mahala pa kazi.
Amewataka wajumbe wa
baraza wa Tume ya Kurekebisha Sheria kuzingatia suala la nidhamu kazini,
misingi ya kazi na kutekeleza majukumu kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu.
Aidha, alitaka uzembe kazini upigwe vita na suala la kufanya kazi kwa mazoea
kukomeshwe na kubainisha kuwa,vipaumbele viwekwe katika kulinda rasilimali za
Tume na kuwa na nidhamu katika matumizi ya fedha na mali zake.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria ambaye ni
Katibu Mtendaji Tume Casmir Kyuki alisema katika kipindi cha Julai 2017 hadi
Machi 2018 Tume yake imeweza kutekeleza majukumu yake kama yalivyoainishwa
katika bajeti.
Ameyataja majukumu hayo
kuwa ni kufanya mapitio ya Mfumo wa Sheria Unaosimamia Haki Jinai, Sheria ya
Ushahidi, Uchambuzi wa Kesi za Mahakama ya Rufaa, Mfumo wa Sheria Unaosimamia
Huduma ya Ustawi wa Jamii, Mfumo wa Sheria za Ufilisi pamoja na kutoa elimu ya
sheria kwa umma.
Ameishukuru serikali
kwa mabadiliko makubwa iliyoyafanya katika sekta ya sheria kupitia tangazo la
serikali namba 48,49 na 50 ambapo yameleta muundo mpya kwa kuanzishwa Ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai na ile ya Wakili Mkuu wa Serikali ili kuongeza
tija na ufanisi katika utendaji kazi.
0 comments:
Post a Comment