Na Robert Hokororo, Ofisi ya Mkurugenzi
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Aggrey Mwanri anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la utunzaji wa misitu litakaloambatana na Maadhimisho ya Upandaji Miti kitaifa wilayani Kishapu.
Akitoa taarifa kuhusu kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Mhe. Nyabaganga Taraba alisema kuwa litafanyika Aprili 4 mwaka huu ambapo wageni mbalimbali wanatarajiwa kushiriki.
Mhe. Taraba ambaye pia Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo Alisema kuwa washiriki watapata elimu kupitia mada mbalimbali kuhusu misitu zitakazotolewa na watoa mada kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Miongoni wa washiriki ni pamoja na viongozi wa Wilaya na Halmashauri zote za Mkoa wa Shinyanga, wataalamu wa misitu nchini, wataalamu kutoka Halmashauri mbalimbali na wananchi.
Aliwakaribisha wananchi kushiriki ili kupata elimu kuhusu umuhimu wa utunzaji miti katika siku zote tatu za maadhimisho kuanzia Aprili 3 hadi 5 mwaka huu katika viwanja vya Shirecu wilayani Kishapu.
Alisema maadhimisho yataambatana pia na maonesho ya bidhaa za misitu pamoja na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali ambapo vyote hivyo vinatarajiwa kuoneshwa katika viwanja hivyo.
Katika kilele cha maadhimisho hayo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla ambapo kauli mbiu ni ‘Tanzania ya Viwanda inawezekana, panda miti kwa maendeleo ya Viwanda’.
Miongoni mwa shughuli zinazotarajiwa kufanyika ni pamoja na zoezi la upandaji miti na kuwa kila kaya itakabidhiwa miche kwa ajili ya kuipanda katika maeneo yao na kutakiwa kuitunza.
Upandaji miti utafanyika vijiji vya Mwatuju na Songwa ambapo lengo la zoezi hilo ni kuifanya Wilaya ya Kishapu kuwa ya kijani kwa kuondoa hali ya jangwa inayoinyemelea.
Sanjari na upandaji miti pia madhimisho hayo yataambatana na utoaji wa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa wananchi ili kujenga uelewa wa umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.
Mhe. Taraba alitumia nafasi hiyo kuwahimiza wananchi kuendelea kupanda miti katika maeneo yao na kuitunza ili kuendelea kuhifadhi mazingira na kuepusha mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame.
0 comments:
Post a Comment