12 March 2018
Katika shughuli za kukagua na kufuatilia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM Mwaka 2015 - 2020, Mkoa wa Kigoma Wilaya Kakonko asubuhi hii Ndg. Humphrey Polepole ameshiriki ujenzi wa zahanati katika kata ya Gwanumpu Kijiji cha Lusenga, ujenzi ambao umeanzishwa kwa nguvu za Wananchi ambapo Ndg. Polepole ameelekeza Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko kutenga fedha kwaajili ya kuunga Mkono Juhudi za Wananchi ili ujenzi wa zahanati hiyo iweze kukamilika kwa haraka.
Ndg. Polepole amechangia nguvu kazi na kiasi cha fedha kwaajili ya ujenzi wa zahanati hiyo.
Aidha Wananchi wameishukuru sana CCM kwa kujitoa na kuwasaidia katika ujenzi wa zahanati na wametoa kilio chao kuwa Mbunge wa Jimbo la Kakonko hakuwapa ushirikiano hata kidogo kwa sababu za kisiasa na ubinafsi.
Wakati huo uo Ndg. Polepole ameshiriki ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Gwanumpu kata ya Gwanumpu ambapo amejitolea nguvu kazi na kiasi cha fedha na amewataka wanafunzi
kusoma kwa bidii na Wananchi waendelee kukiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa kinafanya siasa za maendeleo zinazohusu kushughulika na shida watu.
"Chama chetu tunafanya siasa za maendeleo, siyo siasa za malumbano, matukio na madaraka kama wengine, " alisema Ndg. Polepole
Akiendelea na ziara hiyo Ndg. Polepole ametembelea Ujenzi wa jengo la Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko katika kata ya Kakonko na amesisitiza ulazima wa CCM kufuatilia kwa ukaribu thamani ya ujenzi katika miradi ya serikali ili iendane na gharama halisi za fedha katika miradi.
Katika hatua nyingine Ndg. Polepole ametembelea mradi wa Maji katika kata ya Mgunzu Kijiji cha Nyagwijima ambapo amekuta mradi huo wa Maji ukiwa umekamilika lakini hautoi maji hivyo kutokuwa na manufaa kwa wananchi.
Ndg. Polepole ameelekeza serikali kupitia wizara ya Maji na Umwagiliaji kufika Wilaya ya Kakonko ili ipatie ufumbuzi miradi ya Maji ambayo siyo msaada kwa wananchi na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria wote ambao watakuwa wamehusika kukwamisha miradi hiyo.
"Wizara ya Maji ilete timu ilikurekebisha miradi ya Maji iliyopo na wale waliofanya ubadhilifu wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria". amesisitiza Ndg. Polepole
Huu ni muendelezo wa Ziara ya Kijiji kwa Kijiji Kata kwa kata na Kazi inaendelea ya kukagua na kufutialia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi, CCM Imara ipo Kazini.
Imetolewa na,
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI
0 comments:
Post a Comment