METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, March 9, 2018

WANANCHI WAMKABIDHI VITI NA MEZA DIWANI NYASAKA

Wananchi wa Kata ya Nyasaka wamemkabidhi Jumla ya Viti 50 na Meza 50 Diwani wao Mhe Shaban Ramadhan Maganga kwaajili ya Shule ya Sekondari Nyasaka ili kupunguza changamoto ya uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia kunakoenda sambamba na Sera ya Serikali ya ‘ELIMU BURE’  yenye lengo la kutoa elimu bora, kuboresha mazingira yake na kwa gharama nafuu

Akizungumza katika makabidhiano hayo kwa niaba ya Wananchi, Katibu wa Wazazi wa Shule ya  Sekondari Nyasaka Bi Mabo Chalomola amesema kuwa wameamua kuiunga mkono Serikali katika Sera yake ya ‘Elimu Bure’ kwa kumkabidhi Diwani wao viti na meza kupunguza adha na changamoto inayowakabili wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo ya upungufu wa viti na meza huku wakisisitiza kuwa jukumu la kuboresha mazingira ya utoaji elimu si la kuiachia serikali peke yake

‘ Sisi kama wananchi tumeguswa na adha inayowakabili wanafunzi wanaosoma katika shule yetu, kwa pamoja tukaona ipo haja ya kutoa mchango wetu angalau kupunguza tatizo hili na tunawaomba wananchi wengine waone jukumu hili si la kuiachia serikali peke yake lazima na sisi wananchi tutoe mchango wetu hivyo tunamuomba mheshimiwa diwani aupokee mchango wetu kuunga mkono jitihada za serikali za kutoa elimu bure’ Alisema

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Nyasaka Mhe Ramadhan Maganga mbali na kuwashukuru wananchi hao amewataka kutoishia tu kwenye viti na meza, Kwani hao kama Kata wameshajenga misingi ya madarasa matatu kati ya tisa kwa kata nzima na tofali za kuanzia zipo hivyo amewaomba kuendelea kuunga mkono jitihada za kukamilisha majengo hayo mapya ili kuwafanya wanafunzi wanaosoma katika shule hiyo kupata elimu bora zaidi katika mazingira mazuri

Nae mwalimu mkuu wa shule hiyo Emanuel Bunyinyiga ameahidi kuvilinda na kuvitunza viti na meza hizo huku akitaja changamoto nyengine mbalimbali zinazoikabili shule yake nakuwataka wananchi  hao na viongozi kuendelea kuguswa na changamoto za shule yake

Makabidhiano hayo yalihitimishwa kwa kufanya harambee ndogo ya uchangiaji wa mifuko ya saruji ili kuanza ujenzi wa madarasa hayo mapya ya shule hiyo kwa haraka ambapo zaidi ya mifuko 16 ilipatikana

‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com