Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto MMh. Ummy
Mwalimu akitoa
maelekezo kwa wakurugenzi nchini Tanzania bara juu ya kutenga fedha za mikopo
kwa wanawake.
Wanawake waliohudhuria maandamano kuelekea uwanja wa Nelson Mandela Mjini Sumbawanga kuadhimisha siku ya wanawake Duniani
Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu ametoa
miezi mitatu kwa wakurugenzi wote nchini kuhakikisha wanatenga asilimia 4 za
fedha za halmashauri kwaajili ya kuwapa wanawake mikopo ili waweze kujikwamua
kiuchumi na kuunga mkono juhudi za serikali katika uchumi wa viwanda.
Amesema kuwa serikali
haitasita kuwawajibisha wakurugenzi watakaokiuka maelekezo ya serikali
yanayolenga kutekeleza ahadi za Mheshimiwa Rais kwa wananchi ili kuwawezesha
wanawake wa mijini na vijijini kiuchumi na hatimae kujiongezea kipato na
kuwezesha uchumi wa viwanda.
“Linapokuja suala la
kuwawezesha wanawake kiuchumi hatutanii, chama cha mapinduzi tumepewa kura na
wanawake wa Tanzania hasa wanawake wa vijijini na tumewaahidi wanawake kwamba
tutawapa mikopo yenye masharti nafuu, kwahiyo pale ambapo mkurugenzi anashindwa
kutenga fedha kwaajili ya kuwapatia wanawake mikopo hatutaelewana, na
tunasubiri mpaka tarehe 30 June 2018 wakurugenzi wote ambao hawajatenga fedha
na kuzitoa kwaajili ya wanawake tutapeleka majina yao kwa Mh. Rais
Dk. John Pombe Magufuli,” Mh. Ummy alisisitiza.
Halikadhalika Mh. Ummy
amepiga marufuku suala la kutoa fedha ndogo kwa kikundi kikubwa cha kinamama
huku akitolea mfano kikundi cha watu sita kupewa 300,000 kuwa haitawasaidia
kinamama hao katika juhudi za kujikwamua kiuchumi na kuongeza kuwa ni heri
fedha hizo zikabaki kwa mkurugenzi ili ifanye shughuli nyingine lakini sio
kuwakwamua kinamama.
Ameyasema hayo katika
maadhimisho ya kilele cha Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika
Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kwa kuanza na maandamano yaliyotokea
ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa hadi katika Uwanja wa mpira wa Nelson Mandela
akiwa ni mgeni rasmi wa sherehe hizo.
Awali akisoma risala
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura ameitaka serikali kuhakikisha
wanafanya marekebisho ya sheria kinzani ili kuendana na mabadiliko ya mfumo wa
maisha kama vile sheria ya ndoa, mirathi, maadili ya jamii na kiwango cha
mchango wa mzazi katika malezi ya familia na watoto huku akitaja mafanikio
kadha ya kufikia idadi ya asilimia 50 kwa 50.
“Kuanzishwa kwa
vikundi na kuunganishwa na taasisi za fedha kama vile NMB, CRDB, Pride, SACCOS
na SIDO kwaajili ya mikopo na vifaa kwaajili ya kufanyia kazi, pia mkoa kwa
kushirikiana na Halmashauri tumeweza kuwatambua wazee 48,732 wakiwemo wanawake
na wanaume pia mkoa unaendelea kufuatilia masuala ya kijinsia dhidi ya watoto,
jumla ya watoto 1,307 walifanyiwa ukatili na mashauri yao yapo polisi, dawati
la jinsia na mahakamani,” Alisema.
Akichukua nafasi hiyo
mbunge wa Sumbawanga Mjini Mh. Aesh Hilally nae alimuomba Mh. Ummy kuona
umuhimu wa kuongeza gari za wagonjwa nae Mh. Ummy alikubali ombi hilo na
kuahidi kutoa gari za wagonjwa mbili, moja ikihudumia hospitali ya rufaa ya
mkoa wa rukwa na nyingine katika kituo cha afya kilichopo manispaa ya Sumbawanga.
0 comments:
Post a Comment