Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye pia ni Naibu waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akisisitiza jambo wakati akizungumza na wafugaji wa Jimbo la bukombe walioshiriki kwenye kikao cha kujadili namna ya kuwa na ufugaji wenye tija katika jamii, Leo 3 Machi 2018. Picha Zote Na Mathias Canal-Wazo Huru Blog
Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye pia ni Naibu waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akiwaeleza bwafugaji namna serikali ilivyo jipanga kwa ajili ya kutenga maeneo ya malisho wakati akizungumza na wafugaji Jimboni kwake Bukombe, Leo 3 Machi 2018.
Baadhi ya wafugaji wakimsikiliza kwa makini Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye pia ni Naibu waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko wakati wa kikao cha pamoja akizungumza na wafugaji Jimboni kwake Bukombe, Leo 3 Machi 2018.
Na Mathias Canal, Geita
Baadhi ya wafugaji wamemlilia Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani
Geita ambaye pia ni Naibu waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko kwa kumtaka
kuwafikishia kilio chao kwa Waziri wa Wizara ya maliasili na Utalii Mhe. Dkt
Khamis Kigwangala juu ya kuwafichua baadhi ya maofisa wa serikali
wanaojinufaisha na mifugo ya wananchi hifadhini.
Manufaa ya maofisa hao na askari wa wanyamapori yanajili kipindi
wanapowakamata Ng'ombe wa wafugaji wanaoingia katika maeneo ya hifadhi ya Taifa
ambapo huwakamata na kuwapiga mnada kwa bei yakutupa tofauti na thamani ya
wanyama hao.
Wananchi hao wametoa malalamiko hayo leo 3 Machi 2018 mbele ya
Mbunge huyo wakati wa kikao na wafugaji wa Jimbo hilo la Bukombe kilichofanyika
katika eneo la shule ya msingi Shibingo katika kata ya Yogelo ikiwa ni siku ya
kwanza ya ziara ya Mbunge huyo katika Jimbo hilo la uchaguzi tangu ateuliwe
kuwa Naibu Waziri wa Madini.
Akizungumza katika kikao hicho Mbunge Biteko alisema kuwa
wananchi wanapaswa kutoa taarifa Mara kwa Mara kwa uongozi wa vijiji ili
kuwabaini maofisa hao wanaofanya kazi kinyume na matakwa ya taratibu na sheria.
Aidha, alisema kuwa wananchi wanapaswa kutambua kuwa kumekuwa na
athari nyingi katika jamii kutokana na kukamatwa Ng'ombe wengi kwa ukiukaji wa
taratibu kwa kuwaingiza kuchunga katika maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya
hifadhi.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha muda mrefu wananchi
walijisahau na kupeleka mifugo yao katika maeneo yasiyoruhusiwa kwa ufugaji
hivyo kutokana na usimamizi hafifu wa sheria wananchi wakadhani kuwa wapo
sahihi kwa kila wafanyalo kumbe sivyo.
Mhe Biteko alisema hakuna kilichobadilika badala yake kumekuwa
na usimamizi madhubuti wa sheria katika kila sekta jambo ambalo linawaumiza kwa
kiasi kikubwa wananchi kwani hawakutegemea jambo hilo katika kipindi hiki.
Akijibu kuhusu serikali kuwatengea maeneo ya malisho wafugaji
hao Mhe Biteko alisema kuwa tangu serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli iingie
madarakani imekuwa na kazi kubwa ya kuondoa mifugo holela kutoka nchi jirani
jambo ambalo limeifanya serikali kushindwa kutenga maeneo hayo ya malisho.
Sambamba na hayo aliongeza kuwa wakati Tanzania inapata Uhuru
1961 kulikuwa na Ng'ombe wasiozidi milioni 10 lakini kwa hivi Sasa kumekuwa na
Ng'ombe zaidi ya elfu 40 hivyo serikali inatumia busara kubwa kutenga maeneo
kwani kumekuwa na wingi wa mifugo lakini maeneo hayajaongezeka bado ni yale
yale.
Alisema serikali imedhamiria kwa kauli moja kuwatoa wananchi
katika ufugaji holela usiokuwa na tija na kuhamia katika ufugaji wenye tija ili
kuwa na faida ya ufugaji huo kwa wananchi wenyewe.
Katika hatua nyingine Mhe Biteko alisisitiza kuwa wakati
serikali inaendelea na utaratibu wa manufaa kwa wakulima kwa kuwatengea maeneo
kwa ajili ya malisho, wakulima hao wanapaswa kuwa wavumilivu sambamba na
kushirikiana na serikali katika zoezi la upigaji chapa mifugo.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment