METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, March 27, 2018

KAIMU DC MANYONI AKABIDHIWA KOMBE LA UBINGWA WA MKOA 2018 NA STAND DORTMUND YA MANYONI

Kaimu mkuu wa wilaya ya Manyoni mkoani Singida mh Miraji Mtaturu amepokea kombe la ubingwa wa mkoa kwa mwaka 2018 lililochukuliwa na timu ya Stand Dortmund ya Manyoni huku akitoa pongezi kwa wachezaji hao kwa  ushindi uliyoipata ambao umeleta heshima kubwa ndani na nje ya  wilaya hiyo.

Akipokea kombe hilo leo ofisini kwake wilayani humo mh Mtaturu amesema kama wilaya wana kila sababu ya kuwapongeza kwa ushindi huo unaotoa chachu kwa timu nyingine kuweza kufanya vizuri.

"Niwapongeze sana wachezaji,Viongozi wa timu na wadau wote kwa heshima kubwa mliotupatia, ushindi huu sio wenu peke yenu bali ni ushindi wa wilaya nzima, ahsanteni  na hongereni sana,"alipongeza mh Mtaturu.

Katika kuuunga mkono zaidi juhudi hizo mh Mtaturu ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Ikungi mkoani humo  amechangia shilingi milioni 1  na kuahidi kuwatafutia kocha mzuri zaidi ili  awaandae wachezaji kwa ajili ya mashindano yanayokuja.

Katibu wa timu hiyo  Mohamed Bodalin akitoa neno la shukrani amesema  ushindi walioupata ni matokeo ya ushirikiano mzuri walioupata.

"Tunakushukuru sana mkuu wetu wa wilaya na ofisi yako kwa kutupokea na kwa misaada mbalimbali uliyoitoa kupitia ofisi yako ambayo kwa namna moja ama nyingine imepelekea kutwaa ubingwa huu,kwa sasa tunaenda hatua ya kanda ili kusaka nafasi ya kucheza ligi daraja la pili, tumeandaa bajeti ya sh milioni 20 tunaomba utuunge mkono,"aliomba katibu huyo.

Kwa upande wake katibu wa
Chama Cha Mpira wilaya Joshua Msemakweli amewashukuru Wadau wote walioisadia timu hiyo hadi kufikia hatua ya kutwaa ubingwa wakiwemo  Ofisi ya mkuu wa wilaya, halmashauri ya Itigi, makampuni ya mabasi Super mamuu ya Manyoni, CCM Wilaya,Baba paroko  Padre Wambura wa parokia ya Manyoni, waandishi wa habari  na wadau wote.

Michango mingine iliyopatikana ni sh milioni 1.6,mchele kilo 100, vifaa vya michezo jezi set 3 na viatu vya kuchezea mpira jozi 5.

Mwisho.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com