WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mrajisi wa Ushirika Dkt. Titto Haule aangalie kwa umakini utendaji na ufanisi wa chama cha Ushirika cha MAMCU na viongozi wote ili kubaini kama wanakidhi makusudio yake
Amesema ikiwezekana chama hicho kivunjwe ili waanzishe vyama kilele viwili vitakavyoweza kuhudumia wakulima katika maeneo yao ili waweze kuongeza tija.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo leo (Jumanne, Februari 27, 2018) wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Chiungutwa wilayani Masasi.
Pia Waziri Mkuu amerudia kutoa agizo hilo alipozungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Newala na Halmashauri ya wilaya ya Newala.
Amesema anapata mashaka kuhusu uwezo wao wa kuwahudumia wakulima, hivyo ameagiza kuharakishwa kwa utekelezaji wa agizo hilo ili kurahisisha utoaji wa huduma.
MAMCU inahudumia wakulima wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Manispaa ya Mtwara, Halmashauri ya Nanyamba, Nanyumbu na Halmashauri ya wilaya ya Masasi.
Amesema kwa takwimu hizo haamini kama chama hicho kina uwezo wa kuhudumia maeneo hayo, hivyo kusababisha wakulima kutofikiwa kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaagiza wakulima wa korosho wajiwekee akiba ya fedha ili ziweze kuwasaidia katika ununuzi wa pembejeo.
Amesema kwa mwaka huu Serikali haitogawa pembejeo ya salfa kwa sababu mwaka jana iligawa bure ili kuwahamasisha wakulima kufufua zao hilo.
Kadhalika amewataka wakulima wa korosho wapande miche mipya ya mikorosho na kuiondoa mikorosho ya zamani iliyozeeka ili waweze kuzalisha mazao bora.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, FEBRUARI 27, 2018.
0 comments:
Post a Comment