METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, February 27, 2018

MANAIBU WAZIRI MAVUNDE NA BITEKO WAWASHA MOTO SHINYANGA, WAAJIRI ZAIDI KUFIKISHWA MAHAKAMANI

Na Mwandishi Maalumu, Shinyanga

Manaibu Waziri Anthony Mavunde(Kazi,Vijana na Ajira) na Dotto Biteko(Madini) leo wamefanya ziara ya pamoja katika wilaya za Kishapu na Shinyanga Mjini katika mkoa wa Shinyanga kwa kutembelea migodi ya Madini na Waajiri mbalimbali kwa lengo  la kufuatilia utekelezaji wa sheria mbalimbali za nchi.

Manaibu Waziri hao walianza ziara yao katika Kampuni ya Uchimbaji wa Almasi ya EL HILAL MINERALS LTD iilyopo Wilayani Kishapu ambapo Mh Mavunde aliipa kampuni hiyo siku kumi na nne(14) kuanzia tarehe ya leo wawe wamejisajili katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi(WCF) na kuwataka kulipa  adhabu ya 10%  kwa mwezi kwa kila mchango uliocheleweshwa tangu Julai,2015,Aidha Mh Mavunde pia ameipa Kampuni hiyo siku thelathini(30) kulipa kima cha chini cha mshahara wa sekta ya madini na kutoa mikataba inayokidhi matakwa ya Sheria Na. 6/2004.

Naye Naibu Waziri wa Madini Mh Dotto Biteko ameitaka Kampuni hiyo ya EL HILAL MINERALS LTD kufukia mashimo ili kurudisha mazingira katika hali yake ya mwanzo,kulipa madeni ya mrabaha ifikapo tarehe 21.03.2018,kuandaa mpango wa Uchimbaji na mpango wa Corporate Social Responsibility.

Wakati huo huo Naibu Waziri Mavunde ameagiza kufikishwa Mahakamani kwa Hospital ya Kolandoto na Chuo cha St Joseph Kampasi ya Shinyanga kwa kushindwa kujisajili katika Mfuko wa Fidia wa Wafanyakazi ambapo kwa Mujibu wa Kifungu cha 71(4) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Mwajiri ambaye hajajisajili na mfuko akikutwa na hatia na mahakama atawajibika kulipa faini isiyozidi Tsh 50,000,000 au kifungo kisichozidi miaka mitano jela au vyote kwa Pamoja.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com