METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, January 28, 2018

CCM YAAHIDI KUISIMAMIA SERIKALI YAKE ILI IWAPATIE WANACHI MAENDELEO

Leo tarehe 28 Januari 2018, katika mikutano ya kampeni ya uchaguzi mdogo, Jimbo la Siha katika  Kata ya Ndumeti na Ormelili Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Ndg. Humphrey Polepole, amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitahakikisha Wananchi wa jimbo la siha wanapatiwa na serikali zaidi ya ekari 6000 kwaajili ya ujenzi wa makazi mapya, kilimo na ufugaji.

Mikutano hiyo imehudhuriwa na maelfu ya wananchi pamoja na viongozi mbalimbali wa Chama wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro Ndg. Patric Peter Boisafi.

Mkutano wa Kampeni Kata ya Ormelili

Katibu Mwenezi wa CCM akiwa katika mkutano wa kwanza uliofanyika katika Kata  ya Ormelili wakati akimnadi Mgombea Ubunge wa CCM Ndg. Godwin Mollel, Ndg. Polepole amewaahidi wananchi wa Kata ya Ormelili kuwa CCM itasimamia vyema upatikanaji wa umeme kupitia mradi wa REA awamu ya tatu na matumizi ya eneo la Kilelepori kwaajili ujenzi wa shule, makazi na malisho ya Mifugo yao katika Kata  ya Ormelili.

Aidha, wakati uo huo katika mkutano wa kampeni Kata ya Ormelili viongozi wa CHADEMA wa kata hiyo wamejivua nafasi zao za uanachama na kuomba kujiunga na CCM.  Ndg. Polepole amewapokea na kuomba viongozi ngazi ya Kata na Matawi wawapatie utaratibu wa kuwa wanachama wa CCM.

Mkutano wa Kampeni Kata ya Ndumeti

Akiwa katika mkutano wa pili, Kata ya Ndumeti Ndg. Polepole amewahakikishia wananchi wa Wilaya ya Siha kuwa, CCM ipo kwa ajili ya kuwasemea wananchi na kushughulika na shida zao ikiwemo kuhakikisha Serikali ya CCM inatatua changamoto za wananchi. Hivyo, Ndg. Polepole amesisitiza CCM itaendelea kuisimamia serikali ili ishughulike ipasavyo na tatizo sugu la ardhi kwa kuhakikisha wananchi wanapatiwa hekari  4000 kwa ajili ya makazi, kilimo na malisho ya mifugo yao.

Mkutano wa ndani wa Kampeni Kijiji cha Roseline

Ndg. Polepole amehitimisha mikutano yake katika kijiji cha Roseline Kata ya Ndumeti  ambapo amesema CCM ni Chama Imara, Madhubuti, chenye Sera na Uongozi mzuri hivyo changamoto za Kijiji hicho ambazo ni Zahanati, eneo la kilimo, umeme na michezo, CCM kupitia serikali yake itazipatia ufumbuzi wa haraka na wakudumu.

Akizungumza katika mikutano hiyo Ndg.Polepole amesema Serikali ya CCM itapata wepesi wa kushughulika na shida hizo endapo wananchi watamchagua Dr. Mollel ambaye anaaminika, mwenye uwezo na utayari wa kuwasaidia wananchi.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kimeendelea na mikutano yake ya kampeni ya kuwanadi wagombea wake kuelekea Uchaguzi Mdogo unaotarajiwa kufanyika tarehe 17 Februari 2018.

Imetolewa na,

IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)

SIHA, KILIMANJARO.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com