Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe Mhandisi Elias John Kwadikwa amefanya ziara ya kuitembelea halmashauri ya manispaa ya Ilemela ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu ya barabara inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli katika halmashauri mbalimbali nchini ikihudhuriwa pia na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Ilemela, Madiwani wa Manispaa ya Ilemela na Wataalamu wa wakala wa barabara mkoa wa Mwanza TANROADS
Akiwa Ilemela Mhe Naibu Waziri wa Ujenzi amekagua miundombinu ya barabara ya kutoka Sangabuye kupitia Kabusungu kwenda Igogwe, kutembelea kata ya Kayenze kutakapojengwa gati ya Kivuko cha Usafirishaji kwenda Kisiwa cha Bezi, kutembelea daraja la Msumbiji kata ya Kawekamo, kutembelea daraja la Kigala kata ya Buswelu, kutembelea barabara ya Nyamhongolo na barabara ya kutoka Buswelu Kati kwenda Kiwanda cha Coca Cola Nyakato huku akisema kuwa Serikali kupitia Wizara yake itaendelea kuboresha na kuimarisha miundombinu ili kusaidia wananchi sanjari na kupongeza ushirikiano wa viongozi wa wilaya ya Ilemela katika kutatua changamoto za wilaya hiyo hasa katika suala zima la miundombinu na kuwahakikishia kurekebisha changamoto zote za kimiundombinu zilizoelekezwa katika ofisi yake kupitia wakala wa Serikali wa barabara za mijini na vijijini TARURA
‘… Niwashukuru kwa kuwaona kwenye utatuzi wa matatizo mko pamoja na mnashirikiana, niseme tu mheshimiwa mbunge wenu Dkt Angeline Mabula amekuwa akizungumzia sana juu ya ubovu wa barabara za huku mpaka nikapata shauku ya kuja kujionea ili wakati tunazungumzia utatuzi wake wote tuwe kwenye picha moja, Na wenzetu wa TARURA teyari wameshawasilisha barabara zote zenye changamoto na tunazoteyari mkononi na TANROADS pia wapo niwahakikishie tu utoaji huduma kwa wananchi kwetu ni jambo la kipaumbele …’ Alisema
Akimkaribisha naibu waziri wa Ujenzi mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula mbali na kuomba kuongezwa kwa fedha za mfuko wa barabara amemshukuru kwa ziara yake huku akimuomba kuitazama Ilemela kwa jicho la pekee katika suala zima la kimiundombinu kufuatia upya wake tangu kuanzishwa kwa manispaa hiyo
Kwa upande wake Meneja wa TARURA wilaya ya Ilemela Mhandisi Fuko Koyoya akisoma taarifa yake kwa niaba ya Mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela John Wanga amefafanua juu ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara na madaraja na kuhitimisha kwa changamoto na mpango kazi wa utatuzi wake
' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga '
Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
31.12.2017
0 comments:
Post a Comment