METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, December 20, 2017

JAFO AHIMIZA MIKOA KUSIMAMIA LISHE ILI KUPUNGUZA UDUMAVU

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo (Mb) akimpatia Mkataba wa Huduma za Lishe Naibu Waziri OR TAMISEMI, Joeseph George Kakunda baada ya zoezi la kupitia na kusaini Mkataba wa Utendaji kazi na Usimamizi wa shughuli za Lishe kwa kila mkoa, kikao kazi kilichofanyika mjini Dodoma
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo (Mb) akimpatia Mkataba wa Huduma za Lishe Naibu Waziri OR TAMISEMI, Josephat Sinkamba Kandege baada ya zoezi la kupitia na kusaini Mkataba wa Utendaji kazi na Usimamizi wa shughuli za Lishe kwa kila mkoa, kikao kazi kilichofanyika mjini Dodoma
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu Mawaziri OR TAMISEMI na Wakuu wa Mikoa baada ya zoezi la kupitia na kusaini Mkataba wa Utendaji kazi na Usimamizi wa shughuli za Lishe kwa kila mkoa, kikao kazi kilichofanyika mjini Dodoma
 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo (Mb) akimpatia Mkataba wa Huduma za Lishe Mwenyekiti wa  Wakuu wa Mikoa, Mhandisi Evarist Ndikilo (Mkuu wa Mkoa wa Pwani) baada ya zoezi la kupitia na kusaini Mkataba wa Utendaji kazi na Usimamizi wa shughuli za Lishe kwa kila mkoa, kikao kazi kilichofanyika mjini Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo (Mb) akisani Mkataba wa Utendaji kazi na Usimamizi wa shughuli za Lishe kwa kila mkoa, kikao kazi kilichofanyika mjini Dodoma. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe Lt. Mstaafu Chiku Galawa na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo, na waliosimama ni Naibu Mawaziri na Watendaji OR TAMISEMI wakishuhudia zoezi hilo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo (Mb) amewaongoza wakuu wa Mikoa yote Tanzania Bara, kupitia na kusaini Mkataba wa Utendaji kazi na Usimamizi wa shughuli za Lishe kwa kila mkoa, kikao kazi kilichofanyika mjini Dodoma.

Akiongea na Wakuu wa Mikoa katika ofisi za Wizara hiyo mjini Dodoma, Mhe. Jafo amesema maelekezo hayo awali, yalitolewa na Mhe. Makamu wa Rais wa Tanzania Mama Samia Suluhu, kuhusu tatizo la Lishe katika Mikoa nchini ambalo nchi imekwishajitoa kulishughulikia na kutenga fedha katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2017/2018.

“Tumesaini hii mikataba kwa lengo kubwa la kuhakikisha kwamba Wakuu wa Mikoa kama ndio viongozi wa Wakuu wa Mikoa, wahakikishe halmashauri zao zinaenda kutekeleza mipango yao ya bajeti ambayo imetengwa katika halmashauri zao kwa lengo kubwa kwamba, tunaenda kutekeleza tatizo la lishe ndani ya halmashauri zetu”

Mhe. Jafo amesema Wakuu wa Mikoa wanayo dhamana kubwa ya kusimamia miradi ya maendeleo kama ujenzi wa vituo vya afya na suala la lishe kwa ujumla, hivyo Watendaji watoe taarifa zao kwa Wakuu wa Wilaya kabla ya kuwasilishwa kwa Wakuu wa Mikoa kwa hatua stahiki.

“Wakurugenzi watoe taarifa kwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Wilaya nao wawasilishe kwa Wakuu wa Mikoa ili waone namna ya kuzisemea taarifa hizo”, katika suala zima la utekelezaji wa mipango ya Serikali.

Aidha, amewataka Wakuu wa Mikoa kuwaelekeza na kuwasimamia Wakurugenzi wa Halmashauri kwa ajili ya masuala ya lishe na ujenzi wa vituo vya afya kwani mpaka sasa jumla ya vituo 2011 vimepanuliwa na kujengwa ili kutoa huduma bora kwa jamii.   
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Kebwe S. Kebwe amesema, anaipongeza Serikali kwa kutoa takribani shilingi 11.6 Bilioni kwa ajili ya suala la lishe hasa katika kipengele cha udumavu.

Aidha, amesema suala zima la upatikanaji wa chakula mkoani Morogoro sio tatizo bali ni elimu ya ulaji chakula ndiyo inapaswa kutolewa ili kupunguza utapiamlo lakini pia kumekuwepo na tatizo la Maafisa Lishe katika halmashauri nchini kupangiwa kazi nyingine, kwa mfano kufanya kazi ya Idara tofauti kama vile kukusanya kodi.


Naye Stephen Motambi, Kaimu Mkurugenzi anayeshughulikia masuala ya Lishe Ofisi ya Rais TAMISEMI, amesema suala la Lishe limekuwa likifanyika katika Mikoa na Halmashauri zote katika kukabiliana na tatizo hili lakini kwa hivi sasa hali ya udumavu ni asilimia 34 hivyo mikoa inapaswa kuweka mikakati kuhusiana na kuondoa kabisa tatizo la lishe. 
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com