METDO Tanzania

METDO Tanzania

Wednesday, December 13, 2017

HOTUBA YA RC DODOMA KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO WA UTELEKEZAJI WA RANDAMA YA MAKUBALIANO (MoU)




Mwakilishi wa Mkurugezi wa Misitu na Nyuki, Deusdedit Bwoyo
Mkurugezi kutoka TAMISEMI, Eng. Enock E. Nyanda
Mtendaji Mkuu wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo
Wakuu wa wilaya,
Katibu Mtendaji wa Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF), Dr. Tuli Msuya
Mameneja na Maafisa Misitu,
Wanahabari
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana.

Ndugu Washiriki,

Awali ya yote Napenda kushukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika salama katika kikao hiki muhimu. Aidha, napenda kuwakaribisha katika Mkoa wa Dodoma na kuwatakia makazi mema wakati wote mkiwa hapa. Daima ni faraja na furaha kwetu kuwa nanyi katika mkutano huu. Isitoshe kwasasa tunao uzoefu wa kupokea wageni wa aina mbalimbali na kutoka sehemu mbalimbali. Aidha tunayo miundo mbinu ya kutosha kuwawezesha kuishi hapa kwa amani na kufanya kazi zenu kwa ufanisi mkubwa.



Ndugu washiriki,
Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru Wakala wa Haduma za Misitu Tanzania kwa kuandaa Mkutano huu, ambao ndio nguzo muhimu ya utekelezaji wa Randama ya makubaliano. Kushiriki kwenu kwa wingi katika Mkutano huu ni ishara njema ya kutimiza azma ya hutatua changamoto zinazokabili sekta ya Misitu Tanzania.

Ndugu washiriki,
Nimeambiwa washiriki watakuwa ni Mameneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Maafisa Misitu wa Wilaya na Washauri wa Maliasili wa Mikoa inayounda Kanda ya Kati (Dodoma, Manyara na Singida). Aidha washiriki wengine ni  Wakurugezi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na Menejimenti ya Wakala wa Huduma za Misitu kutoka Makao Makuu.
 Nimeelezwa pia kwamba madhumuni ya mkutano huu ni utekelezaji wa Randama ya makubaliano iliyosainiwa kati ya Wizara ya Maliasili na Utalii na Ofisi ya Raisi TAMISEMI ili kuimarisha usimamizi wa Misitu nchini na utawala bora, kufanya uperembaji wa miradi inayofadhiliwa na mfuko wa misitu Tanzania na  kuboresha ukusanyaji, ugawaji, utumiaji na ufuatiliaji wa matumizi ya asilimia tano ya tozo ya upandaji miti.

Ndugu Washiriki,
Katika mkutano huu mtapata nafasi ya kushiriki, kusikiliza na kujadiliana kwa kina mada zifuatazo:- Hali ya usiamizi wa misitu Tanzania; utekelezaji wa Maazimio ya kikao cha kwanza cha Ushirikiano; Taratibu za uvunaji na usafirishaji wa mazao ya misitu kutoka misitu ya Asili; Randama ya makubaliano na Ufafanuzi wa sheria; Utekelezaji wa Makubaliano ya kuboresha ukusanyaji, ugawaji matumizi na Ufuatiliaji wa 5% fedha za tozo ya upandaji miti.

Ndugu washiriki;
Kama mnavyofahamu Misitu ya Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa mbili;-
i.             Uharibifu mkubwa wa misitu unaofikia kiasi cha hekta 372,000 kwa mwaka,
ii.            Mahitaji ya mazao ya misitu kwa mwaka kuzidi uwezo wa misitu kwa zaidi ya meta za ujazo milioni 19.5.

Changamoto za usimamizi wa misitu zilizopo Kanda ya kati ni Pamoja na:
1     Uvunaji holela wa mazao ya misitu na biashara ya mazao hayo isiyofuata Sheria na taratibu.
2     Utegemezi mkubwa wa misitu kwa ajili ya nishati (mkaa na kuni)
3     Ukataji ovyo wa miti unaotokana na kilimo cha kuhamahama hususan kwa ajili ya kilimo, makazi na biashara.
4     Uchomaji holela wa moto katika maeneo ya misitu
5     Kuongezeka kwa mahitaji ya mazao ya misitu yanayotokana na kuongezeka kwa watu na kiwango kidogo cha upandaji wa miti.
6     Rasilimali za misitu kuwa katika Usimamizi wa wadau mbalimbali bila uratibu imara.
7     Uvamizi wa misitu ya hifadhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji wa mifugo.
8     Uchache  wa vitendea kazi (magari na pikipiki).
9     Uchache wa Rasilimali watu (na baadhi ya watumishi sio waaminifu).

Ndugu washiriki,
Faida za Misitu kitaifa na kimataifa zinajulikana ikiwa ni [pamoja na kuhifadhi udongo, upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali, ufugaji wa nyuki hivyo upatikanaji wa asali, nishati, upatikanaji wa mvua, na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi. Hivyo juhudi za pamoja zinatakiwa katika kulinda na kuhifadhi misitu yetu. Kwa kulitambua hili, ndio maana Wizara mbili; Maliasili na Utalii  na Ofisi ya Raisi – TAMISEMI zilisaini Randama ya makubaliano ili kuunganisha nguvu pamoja katika kuzikabili changamoto zinazokabili sekta ya Misitu hapa nchini.

Ndugu washiriki,
Napenda kuchukua fursa hii pia kuwaasa watumishi wa misitu chini ya TFS na wa Tamisemi ambao ndio watekelezaji wakuu wa Randama katika ngazi za Wilaya kutekeleza kikamilifu maelekezo yote yaliyopo katika Randama ya Makubaliano iliyosainiwa na Wizara hizi mbili ili kufikia malengo tarajiwa kwa ufanisi zaidi.

Ndugu washiriki,
Katika mkutano huu pamoja na mambo mengine mtajadili masuala mbalimbali kuhusu Usimamizi wa misitu na majukumu ya kila mdau katika kuhifadhi na kulinda misitu iliyopo Kanda ya Kati. Nimatumaini yangu na ninawasihi kwamba mikakati na maazimio mtakayojiwekea haitabaki katika mashelfu/makabati katika ofisi zenu bali itakuwa kwenye utekelezaji wa kazi zenu za kila siku. Aidha, nashauri mikakati mtayopanga ilenge kuwashirikisha wananchi katika Usimamizi wa Rasilimali za Misitu hapa nchini kwa malengo na matumizi endelevu.

Ndugu washiriki,
Kwa kuzingatia umuhimu wa hifadhi za misitu nchini, ni vyema kila mwananchi akazingatia maagizo ya Serikali pamoja na kufuata sheria za nchi zinazohusiana na uhifadhi na Usimamizi wa Maliasili zetu. Ningependa kuwaasa na kuagiza kuwa ni marufuku mtu yeyote kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya hifadhi za misitu na kama kuna watu wanaendesha shughuli hizo naagiza waondoke mara moja, kabla Sheria haijachukua mkondo wake.

Ndugu washiriki,
Baada ya kusema haya ninatamka rasmi kuwa “Mkutano wa utekelezaji wa  Randama ya makubaliano kuimarisha Usimamizi wa misitu nchini na utawala bora baina ya Wizara ya Malisili na Utalii na Ofisi ya Raisi TAMISEMI” umefunguliwa rasmi.

ASANTE SANA KWA KUNISIKILIZA
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com