METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, December 10, 2017

DC BUSEGA MHE TANO MWERA AJIPANGA KUMALIZA TATIZO LA UKATILI WA KIJINSIA

Na Mwandishi Wetu, Simiyu

Mkuu wa Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu Mhe Tano Mwera amejipanga kupunguza na kumaliza kabisa tatizo la ukatili wa Kijinsia katika Wilaya ya Busega. 

Mhe Mwera amebainisha hayo wakati wa kupokea maandamano wakati wa siku ya kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto leo Tarehe 10 Disemba 2017. 

Alisema kuwa tatizo la ukatili wa kijinsia kwa kiasi kikubwa lipo nchini na linaendelea kuongezeka licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali kama vile kufungua madawati ya jinsia katika kila kituo cha polisi.

Pia Alisema kuwa serikali kutoa asilimia tano ya kukopesha wanawake katika vikundi vyao kwa mfano, kuanzia mwezi Januari mpaka Mwezi Juni ndani ya Wilaya ya Busega kesi 14 zimeripotiwa katika dawati hilo la jinsia. 

Aidha, alisema kesi nyingi zinaendelea kuripotiwa kwani mpaka kufikia mwezi Disemba mwaka huu takribani kesi 58 zimeripotiwa.

Mhe Mwera alisema kuwa ukatili wa kijinsia ni jambo ambalo halikubaliki hivyo ni lazima kuzungumzia jambo hilo kama ambavyo kauli mbiu ya mwaka huu inasema "Funguka" ukatili dhidi ya wanawake na watoto haumwachi mtu salama, chukua hatua."

Alikaririwa Mhe Mwera alisema kuwa "Na sisi tufanye hivyo hivyo, Tuhakikishe tunaripoti matukio yote katika dawati la jinsia ili sheria ichukue mkondo wake, pili tuwe tayari kutoa ushahidi mahakamani, na tusikubali kukubaliana na watuhumiwa kwa kupewa pesa kwani tabia hizo ndizo zinazosababisha ukatili wa kijinsia kuendelea, tatu, tuachane na mila na desturi zinazokandamiza wanawake, tuwape nafasi wanawake kutoa maoni na kusikilizwa katika familia"

Alisema wananchi wanapaswa kuachana na imani za kishirikina na mila potofu za kucheza ngoma wakati wa mavuno, ngoma kama Bukwilima na Burabo, ambazo zinasababisha kumaliza chakula na hatimaye mifarakano ndani ya nyumba. 

Vile vile aliwasihi wananchi kutokubali kutoa ama kupokea rushwa huku akitilia msisitizo pia kwa watu wa Usalama kutotoa wala kupokea rushwa.

"Rushwa ni adui wa haki, Na atakaye bainika atachukuliwa hatua kali za kisheria Na kwa wataalamu hakikisheni mikakati yenu ya kutoa elimu kwa jamii kwa  kushirikisha makundi yote wanaume, wanawake, viongozi wa dini, viongozi wa mila, na Taasisi mbalimbali" Aliongeza Mhe Mwera

Alisisitiza wanawake kufanya kazi kwa bidii, na kutumia fursa ambazo zipo kwani kuna majukwaa ya wanawake kutoka katika ngazi ya Kata, Wilaya na Mkoa na huku akiwasishi kujiunga na vikundi kwa ajili ya kujipatia asilimia tano ya mkopo serikalini.

Alisema kuwa katika Kuelekea uchumi wa viwanda hakuna atakayeachwa nyuma kila wananchi anapaswa kufanya kazi kama kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli inavyoelekeza "Hapa Kazi Tu"

MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com