METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, November 5, 2017

Waziri Mwakyembe awataka wataalam wa Michezo kuleta matokeo Chanya katika sekta ya Michezo nchini.

 images
Na Lorietha Laurence-WHUSM

Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka wakufunzi 128 ambao ni wataalam wa michezo kuzingatia kwa makini yote waliojifunza na kuyafanyia kazi ili kuleta matokeo chanya kwenye sekta ya michezo nchini .

Akizungumza katika ufungaji wa mafunzo hayo  Wilayani   Kyela Mkoani Mbeya ambapo Mhe. Dkt. Mwakyemba alieleza kuwa sekta ya michezo ni ajira na chanzo kikubwa cha mapato hivyo wakufunzi hao wakasimamie vyema waliyojifunza na kuyafanyia kazi kwa ajili ya maendeleo ya michezo nchini.

“Michezo ni ajira na chanzo kikubwa cha mapato hivyo msimamie vyema yote mliyojifunza na kuyafanyia kazi ipasavyo ili kuleta matokeo chanya kwa jamii yetu kwa kuwa na wacheza bora wa kimataifa”amesema Mhe. Mwakyembe.

Aidha ameongeza kwa kueleza kuwa mbali ya kuwa michezo ni ajira pia  ni kinga bora inayosaidia katika kuimarisha afya na hivyo kujiepusha na maradhi mbalimbali jambo ambalo ni muhimu kwa jamii.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Bw. Mohamed Kiganja  ameeleza kuwa Baraza lake limejipanga  kutoa mafunzo ya wataalam wa michezo hayo kwa nchi nzima na hivyo kuzishauri Halmashauri kuchangamkia fursa hiyo kwa kujiandaa na kuwasilisha maombi mapema ili kuyafanyia kazi.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kyela. Dkt. Hunter Mwakifuna alimshukuru Waziri Mwakyembe kwa mchango wa hali na mali katika kukamilisha mafunzo hayo na kuahidi kuwatumia wakufunzi hao katika  kufundisha michezo Wilayani hapo.

Nao Wahitimu wameishukuru serikali kwa jitihadi iliyofanta ya  kuwaandalia mafunzo hayo na kuahidi kuwa walimu na mabalozi bora katika sekta ya michezo kwa kuibua na kuendeleza vipaji vya wachezaji katika ngazi mbalimbali.

Mafunzo hayo yalifanywa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ilianza tarehe 23 hadi 28 Oktoba huku awamu ya pili ikiwa ni kuanzia 29 Oktoba hadi tarehe 4 Novemba mwaka huu chini ya uratibu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Chuo cha Michezo Malya cha Mkoani Mwanza lengo ikiwa ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na wataalam wa kutosha katika sekta ya michezo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com