Kuku wakiendelea kuandaliwa ndani ya Soko la Kisutu. Picha zote na MaendeleoVijijini.
Na Daniel Mbega, MaendeleoVijijini
SAUTI
za kuku zinasikika hata ukiwa nje ya jengo dogo ndani ya Soko la Kisutu
jijini Dar es Salaam, lakini ghafla zinakoma na zinasikika nyingine.
Siyo
kwamba kuku hao wanahitaji chakula ama wanacheza, bali hapa ni
machinjio, na sauti zinapokoma ujue tayari zimekwishapigwa kisu na
zinaandaliwa kwa ajili ya kitoweo.
Nje ya jengo hilo unaweza kuwa umekuta akinamama wengi wakiwa wamelundikana huku wakiwa wamekalia ndoo zao.
Hawa nao wanasubiri huduma, wanataka kununua utumbo, miguu pamoja na vipapatio vya kuku hao wanaochinjwa ili wakafanye biashara.
Akinamama
hawa wanatoka katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na hapa
Kisutu ndiko mahali pekee ambako wanaweza kupata bidhaa hiyo
wanayokwenda kuuza mitaani.
Bila
shaka baadhi yetu tumekutana ama tumewakuta akinamama wakiuza firigisi
na utumbo mitaani, basi amini kwamba asilimia kubwa wanapata bidhaa hiyo
katika eneo hili la Kisutu.
Ukiingia ndani ya jengo hilo usishangae ukasalimia usiitikiwe na watu wengi, japokuwa waliomo ni wengi.
Kabla hujajua usimame wapi, utasikia sauti ya mtu akikutaka radhi kwamba anaomba kupita ama anataka kuweka mzigo.
Naam.
Kila mtu hapa yuko ‘busy’ na kazi inakwenda mtindo mmoja, na hata
kutokukuitikia si kwamba wanafanya kiburi ama hawajakuona, la hasha. Kwa
sababu wanataka kuhakikisha kazi wanayoifanya inakuwa katika hali bora
hasa ikizingatiwa kwamba hicho ni chakula kwa afya ya binadamu.
Mazingira ya ndani yanaridhisha kutokana na usafi ambao unazingatiwa sana na wahusika licha ya changamoto za hapa na pale.
Hawa
ni wanaushirika wa Kisutu Poultry Farm Cooperative Society (KIPOCOSO),
ambao wamekuwepo katika soko hilo kwa zaidi ya miaka 28 na ndio
waanzilishi wa kuchinja kuku jijini Dar es Salaam.
Japokuwa
hivi sasa baadhi ya masoko yana machinjio ya kuku, lakini wengi
wanaohusika na uchinjaji wamejifunza ama wamewahi kufanya shughuli hizo
katika Soko la Kisutu.
Kuku walionyonyolewa, kuchunwa ngozi au kukatwakatwa wanaweza kukutoa udenda wangali wabichi na wamewekwa mafungu mafungu.
“Kila
fungu unaloliona hapo lina mwenyewe, hawachanganyani kabisa,” ndivyo
anavyoeleza Bw. Hamisi Malamla, Mwenyekiti wa KIPOCOSO.
Anaongeza:
“Kazi yetu hapa ni kuchinja, kuku wote wana wenyewe na kila mmoja hapa
ndani anakwenda hapo nje kwenye mabanda wanakonunua kuku na kutafuta
oda, akiipata anakuja kuchinja na kuwatengeneza.”
Bw.
Malamla anasema kwamba, asilimia kubwa ya kuku wanaoliwa jijini Dar es
Salaam wanachinjwa na kuandaliwa katika soko hilo, sehemu ambayo pia ni
maarufu kwa wauzaji wa kuku – wa nyama wa kisasa pamoja na wa kienyeji.
Ndani
ya jengo hilo lililowekwa terazo, kujengwa masinki bora pamoja na
majiko matatu makubwa yanayotumia gesi, takriban kuku 3,000 huchinjwa
kila siku.
Licha
ya kufanya shughuli zao kwa ufanisi, lakini unapozungumza na
wanaushirika hawa utagundua kwamba wana mawazo makubwa ya maendeleo
tofauti na unavyoweza kuwadhania.
“Malengo
yetu ni kujikita katika uwekezaji wa kilimo na mifugo, tunataka tuanze
kufuga wenyewe kuku (wa kisasa na kienyeji), kuuza kuku wenyewe,
kutotolesha vifaranga, kutengeneza vyakula vya kuku pamoja na kusambaza
madawa,” anasema Bw. Malamla.
Anasema
kwamba, ikiwa wataanza uwekezaji wa kufuga kuku itakuwa ni hatua kubwa
kwao kwani watakuwa na uhakika wa kuchinja na kuuza, na kwamba oda
wanazozipata kwa sasa zitakuwa ni nyongeza tu na ziada.
Malamla
anasema, kwa uzoefu walionao, ikiwa watajikita pia katika ufugaji
wanaweza kulisha wananchi wengi jijini Dar es Salaam na kwamba hata kuku
watakaowafuga wanaweza kuongezeka ubora tofauti na baadhi ya wanaouzwa
sokoni hapo ambao mara nyingi huwa hawana uzito mkubwa.
“Tukianza
ufugaji ni dhahiri tutaongeza ubora kulingana na mahitaji ya soko na
hatuwezi kubahatisha, kwa sababu hapa wakati mwingine kuku wanaadimika
na inapotokea hivyo maana yake tunakosa kazi ya kufanya,” anasema.
Anaongeza
kwamba, tangu uongozi wake ulipoingia madarakani mwezi Machi 2017
(miezi nane iliyopita) wamefanikiwa kujiwekea akiba ya kutosha ambayo
inawapa msukumo wa kuangalia fursa za uwekezaji ili kuongeza kipato
pamoja na kupanua wigo wa ajira.
0 comments:
Post a Comment