METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, November 25, 2017

MAVUNDE AWANEEMESHA WAJASIRIAMALI DODOMA







Mbunge wa jimbo la Dodoma mjini Anthony Mavunde leo amekabidhi mashine mbalimbali kwa wajasiriamali wa vikundi 31 na kuwataka kuhakikisha wanazitumia kwa kujiongezea kipato na kuenda sambamba na azma ya serikali ya awamu ya tano ya uchumi wa Viwanda.

Akizungumza na wanavikundi hao na wakazi wa Dodoma, Mavunde amesema mashine hizo zimenunuliwa kupitia fedha za mfuko wa jimbo na kwamba dhamira yake ni kuhakikisha wananchi wanajikwamua kiuchumi kwa kubadili maisha yao.

“Leo Tumegawa mashine hizi mkazitumie zibadilishe maisha yenu msizifungie stoo zikajaa vumbi na msipozitumia kwa malengo yaliyokusudiwa hamuwezi kufikia malengo yenu,Mashine hizi zikaunge mkono falsafa ya Rais ya uanzishaji wa viwanda ili kufikia uchumi wa viwanda,”amesema Mavunde

Hata hivyo amewahakikisha kuwa amejipanga kuhakikisha anawakwamua wananchi wake kiuchumi kupitia fursa mbalimbali na kwamba anakuja na mradi wa kuchimba mabwawa ya kufugia samaki.

“Kuna teknolojia imekuja ya kufuga samaki ambayo unaweza kufuga nyumbani, hiyo ndo mipango ya ofisi ya Mbunge ya kuwawezesha wananchi kiuchumi na pia kwa upande wa kilimo nimetafuta wataalamu kutoka India tunaangalia eneo la Nzasa kulitumia kwa majaribio ya kilimo cha mboga mboga na ufugaji samaki,”amesema

Mavunde amesema dhamira yake ni kuwafanya wananchi wa Dodoma wanufaike na ujio wa serikali mkoani humo kupitia fursa mbalimbali za kujikwamua kiuchumi.

Akizungumzia kuhusu kilimo cha Zabibu, Mavunde amewataka kuchangamkia fursa ya kilimo cha zabibu kwa kuwa ni fursa pekee ya kuikwamua kiuchumi Dodoma ikiwa ni pamoja na uanzishaji wa viwanda vidogo vya kukamua mchuzi wa zabibu.

“Maana kwasasa utambulisho wa Dodoma ni ombaomba na wavivu badala ya kutambulika kwa kilimo cha zabibu, ndugu zangu duniani kote Dodoma ni miongoni mwa maeneo yanayovuna zabibu kwa mwaka mara mbili ni vyema tukatilia mkazo kilimo hichi ili kuwa utambulisho wetu,”amesema

Mbunge huyo amesema kupitia mshahara wake anatarajia kununua mashine za kukamua mchuzi wa zabibu kutoka nchini Canada kwa kila kata kwa kuwa mchuzi huo una soko kubwa.

Amewahamasisha wananchi kupitia vikundi walivyo navyo kuendelea kuwasilisha maombi yao na Ofisi ya Mbunge itaendelea kununua mashine kwa awamu.

Naye, Mwakilishi wa Umoja wa wajasiriamali Silvesta Wambura amemshukuru Mbunge huyo kwa dhamira yake ya kuwainua kiuchumi na kudai kuwa amekuwa mkombozi wa wanadodoma.

Amesema Mbunge huyo ni chombo sahihi na mwenye ubinadamu na wananchi wana matarajio makubwa kupitia yeye.

Kwa upande wao, madiwani wa kata za jimbo hilo wamempongeza na kumshukuru Mavunde kwa dhamira yake ya kuwakwamua wananchi kiuchumi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com