Naibu waziri wa maji na umwagiliaji
Jumaa Aweso amewataka wakandarasi nchini kuwa wazalendo katika kuhakikisha
fedha zinazopelekwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji zinafanya kazi
iliyokusudiwa.
Aweso ametoa rai hiyo akiwa katika
kijiji cha Bubutelo wilayani Chemba akiwa katika ziara yake ya kutembelea na
kuzumgumza na wananchi wa vijiji vya Mombose na Bubutelo ambavyo vipo katika
eneo linalotarajiwa kujengwa bwawa la Farkwa.
Aweso amesema serikali inajitahidi
kutenga fedha ili kukamilisha miradi hiyo na hatimaye ifikie azma ya kumtua
ndoo ya maji kichwani kama ilivyokusudiwa hivyo ni wajibu wao kuwa wazalendo.
"Mkandarasi anayepewa kazi
ajione kabisa yeye ni Mtanzania avae uzalendo kwa Taifa lake,serikali inatenga
fedha nyingi za miradi lakini wapo wakandarasi ambao sio waaminifu jambo ambalo
linakwamisha nia nzuri ya serikali iliyonayo,"amesema Aweso.
Katika ziara hiyo Aweso amesikiliza
vilio vya wananchi ambao wengi waliomba kujua hatma ya fidia zao ili wapishe
mradi huo suala ambalo amesema linashughulikiwa na likikamilika kila
anayestahili kulipwa atalipwa.
Kwa upande wake mbunge wa Chemba Juma
Nkamia amesema wananchi wameupokea mradi huo vizuri na wanachosubiri ni fidia
zao na kuwasisitiza wananchi kuwapuuza baadhi ya watu wanaopita na kusema mradi
huo haufai.
Naye kaimu mkurugenzi wa halmashauri
hiyo Jofrey Pima amesema hali ya upatikanaji wa maji ni ndogo ikilinganishwa na
idadi ya watu waliokuwepo ambapo mijini wananchi 4490 ndio wanapata maji
na kijijini ni asilimia 44.
"Bwawa
la Farkwa likikamilika litasaidia kuongeza idadi ya wanaopata maji na hivyo
kukidhi dhamira ya serikali,kwa sasa upembuzi yakinifu umeshafanyika,tunasubiri
suala la kuwalipa fidia wananchi,"amesema kaimu mkurugenzi huyo.
Wilaya ya Chemba ilianzishwa
mwaka 2012 na mwaka 2013 iliundwa halmashauri ambapo ina jumla ya tarafa
4,kata 26 na vijiji 114 ikiwa na jumla ya wakazi laki 256,623 kwa sasa.
0 comments:
Post a Comment