METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, October 26, 2017

WAMACHINGA KARIAKOO WAMPONGEZA NA WAAPA KUMPIGANIA JPM

Ilala, Dar es salaam

Wafanyabiashara ndogondogo (wamachinga) wa Soko la Kariakoo, jijini Dar es salaam Leo wamevunja ukimwa na kupaza sauti zao kumuunga mkono na kumpongeza Rais wa JMT Mhe. John Pombe Magufuli kwa juhudi zake zinazoendelea za kuwatumikia watanzania na kuhakikisha kwamba rasirimali za Tanzania zinatumika kwa manufaa ya taifa. Salamu hizo za pongezi zimetolewa leo katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Wilaya ya Ilala ambapo maelfu ya wamachinga waliamua kufunga biashara zao kwa muda, ili kwenda kufikisha ujumbe wao kwa Waziri wa Madini Mhe. Anjela Kairuki ambaye walimwalika kuwa Mgeni Rasmi.
Akizungumza kwa niaba yao, Katibu wa Umoja wa wafanyabiashara hao alisema;

*“Tunampongeza Mhe. Rais kwa mapambano ya kiuchumi kwa nchi yetu hasa katika sekta ya madini, vita ambayo viongozi wengi wa Afrika wanaiogopa au wanaamua kushirikiana na wageni kuiba rasirimali za nchi kwa maslahi yao binafsi. Lakini kwa Rais wetu imekuwa ni tofauti, ameweka kando malsahi yake binafsi na amejivisha vazi la uzalendo kwa taifa lake. Tangu alipoanzisha sakata la Makinikia hadi sasa ambapo matunda yake yanaonekana wapo waliokejeli, waliombeza na kumkatisha tamaa lakini hakurudi nyuma wala hakuyumbishwa na hatimaye leo Tanzania itaandika historia mpya ya kuwa na mikataba bora katika sekta ya madini ambayo itanufaisha watanzania wenyewe”*

Kuhusu fedha zinazotarajiwa kupatikana kutokana makubaliano yaliyofikiwa katibu huyo alisema, kiwango cha fedha takribani Bilioni 700, ambazo zimeokolewa na Mhe. Rais si haba kwani hatukutarajia kuzipata. Fedha hizi zitasaidia kuboresha huduma mbalimbali zikiwemo Afya, Elimu na miundombinu.

*“Tunamuomba Rais wetu asisikilize kelele za watu wanaombeza kwani wengi wao ni wale ambao hawana uchungu na uzalendo kwa taifa lao. Sisi wananchi wanyonge ambao yeye ndiyo mtetezi wetu daima tuko pamoja naye, bega kwa bega”*

Aidha, wafanyabiashara hao walitumia fursa hiyo kumshukuru Rais kwa maelekezo yake yaliyowawezesha kusajiliwa na kutambulika rasmi kwa kupewa vitambulisho vya NIDA. Chini ya mpango huu takribani wafanyabiashara 4700 tayari wamepatiwa vitambulisho kati ya wamachinga 5400 waliotayari kuingizwa kwenye mpango huo unaoratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala.

Akimkaribisha Waziri wa Madini, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia Mjema aliwashukuru wamachinga hao kwa uamuzi wao wa kutambua kazi inayofanywa na Mhe. Magufuli. *Aliwahakikishia kwamba Wilaya yake na serikali kwa ujumla itaendelea kuwa nao bega kwa bega ili waendelee kufanya shughuli zao kwa mafanikio makubwa*.

Kwa upande wake Waziri Kairuki alieleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kutokana na mjadala uliofanyika kati ya Serikali na Kampuni Barrick na hivyo kuwataka watanzania kuendelea kumuunga mkono na kumtia moyo kiongozi wao ili aendelee na kazi ya kulijenga taifa letu.

Mkutano huo ulihudhuriwa na mbunge wa Jimbo la Ilala Mhe. Zungu, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala ndugu Edward Mpogolo na viongozi wengine.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com