Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mwanza
Kwa kuwa mfumo wa ununuzi wa pamoja umekuwa ukitumika kwa lengo
la kupata mbolea kwa bei nafuu kutoka kwa wazalishaji na kwa kuwa mazingira ya
sasa duniani yanaonesha kuwa mfumo wa ununuzi wa pamoja hauwezi kukidhi
mahitaji hayo hivyo Wizara ya Kilimo imeamua kuruhusu ushindani li kila mwenye
uwezo wa kuleta mbolea na kuiuza afanye hivyo ili mbolea iwepo nchini kwa wingi
na bei shindani.
Uamuzi huo wa serikali kuruhusu kila mfanyabiashara kuagiza
mbolea itaifanya Tanzania kuwa kitovu (HUB) cha mbolea kwa matumizi ya ndani na
nchi zinazoizunguka.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda ametoa msimamo huo wa
serikali leo tarehe 4 Julai 2021 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
wakati alipofanya ziara ya siku moja katika Ofisi za Bodi ya Pamba Jijini
Mwanza.
Amesema kuwa kwa kuzingatia Kanuni ya 7(4) ya Kanuni za Ununuzi
wa Mbolea kwa Pamoja Na. 49 za mwaka 2017, hivyo amewataka wafanyabiashara wote
wenye nia ya kuingiza mbolea nchini kwamba, wako huru kufanya hivyo bila
kupitia zabuni ya uagizaji wa mbolea kwa pamoja.
Waziri Mkenda amesema kuwa Katika kufanikisha mpango huo,
Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa ushindani unakuwa wa haki na Wizara ya
Kilimo kwa muda wote itakuwa tayari kushirikiana na Kampuni yoyote itakayoagiza
mbolea.
"Nitoe wito kwa wafanyabiashara wote wa mbolea kuwasilisha
maombi yao ya kuagiza mbolea kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea haraka
iwezekanavyo" Amekaririwa Prof Mkenda
Ndugu Wanahabari, nimewaita hapa ili nizungumze nanyi
kuhusu suala la upatikanaji wa mbolea nchini hususan kwa msimu wa
2021/2022.
Prof Mkenda amesema kuwa upatikanaji wa mbolea hapa nchini
unategemea uzalishaji unaofanywa na viwanda vya ndani na upungufu hufidiwa kwa
kuagiza nje ya nchi kupitia mfumo wa ununuzi wa pamoja (bulk procurement) na
uingizaji unaofanywa na Kampuni za mbolea zinazopatiwa vibali na Mamlaka ya
Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).
Amesema kuwa mahitaji ya mbolea kwa msimu wa 2020/2021 yalifikia
tani 718,051 na upatikanaji ulifikia asilimia 82 hadi mwezi Mei, 2021. Katika
mazingira ya kawaida kipindi cha kati ya Julai na Oktoba kila mwaka watumiaji
wakubwa wa mbolea duniani hupunguza matumizi ya mbolea na hivyo bei katika soko
la dunia hupungua.
Kwa mwaka 2021 hali hiyo imekuwa tofauti na miaka mingine kwa
kuwa bei za mbolea duniani zimeendelea kupanda kutokana na sababu mbalimbali
ikiwemo athari za Ugonjwa wa Homa kali ya Mapafu unaosababishwa na Virusi vya
Corona (COVID-19) ambapo baadhi ya viwanda vimepunguza uzalishaji na
kusababisha bei kupanda kutokana na kuwepo kwa mahitaji makubwa ikilinganishwa
na upatikanaji hususan kwa nchi watumiaji wakubwa wa mbolea.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment