Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema
Nchimbi akiwafundisha uzalendo kwa taifa wanafunzi wa Shule ya Msingi
Mwakichenche iliyoko wilayani Singida kama sehemu ya maadhimisho ya
kumbukumbu ya baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema
Nchimbi akikakua ujenzi wa vyoo katika Shule ya Msingi Mwakichenche
iliyoko wilayani Singida kama sehemu ya maadhimisho ya kumbukumbu ya
baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere. Vyoo hivyo vimejengwa kwa fedha
kutoka serikali kuu kupitia program ya Lipa kutokana na Matokeo.
Kiongozi wa Wanafunzi wa
Sekondari ya Ilongero Daudi William Kihanga akiishukuru serikali kuu
kupitia program ya Lipa kutokana na Matokeo kwa kuwaboreshea miundombinu
ya kujifunzia. Aidha ameshukuru Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema
Nchimbi kwa kuwanunulia chakula (mchele kilo 140) kama sehemu ya
maadhimisho hayo.
..............................................................................................................
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema
Nchimbi leo amekagua miradi ya uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia na
Kufundishia katika shule nne za Msingi na sekondari, kama sehemu ya
kumbukumbu ya Hayati baba wa Taifa la Tanzania Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere.
Katika ziara yake Dkt Nchimbi
ametumia muda mwingi kuwafundisha uzalendo kwa taifa, wanafunzi wa shule
za Sekondari Ilongero na Mtinko pamoja na shule za Msingi Mtinko na
Mwakichenche zote za Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
Dkt Nchimbi amesema, wanafunzi hao
watamuenzi mwalimu Nyerere na kudumisha uzalendo endapo watasoma kwa
bidii ili taifa lipate wataalamu wa kutosha katika Nyanja mbalimbali
watakaoweza kusaidia kukuza uchumi wa Tanzania.
“Mchango wa baba wa Taifa Mwalimu
Nyerere kwa taifa letu ni mkubwa sana kwakuwa licha ya kutupatia uhuru
pia ametukomboa katika umasikini, ujinga na maradhi, hivyo basi nawaasa
muipende sana elimu ili na nyinyi muweze kuwa sehemu ya kulisaidia
taifa”, ameeleza Dkt Nchimbi.
Ameongeza kuwa katika kuboresha
elimu serikali ya awamu ya tano imetoa zaidi ya shilingi bilioni 1
Mkoani Singida kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kidato cha tano na
sita pamoja na kujenga miundombinu ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu
kwa kipindi cha mwaka 2017/2018.
“Tunapomkumbuka Mwalimu Nyerere
leo tuthamini mchango wa serikali yetu unaofanya kwa ajili ya kuboresha
sekta mbalimbali, mfano katika sekta ya elimu shilingi 1,052, 200,000
zilizotolewa nimethibitisha zimefanya kazi nzuri, kazi kwenu walimu
kufundisha kwa bidii na wanafunzi kukazana katika kusoma kwakuwa
mazingira yameboreshwa sana”, amesisitiza Dkt Nchimbi.
Aidha Dkt Nchimbi amewapongeza
wakuu wa shule na kamati za shule hizo kwa kuchagua mafundi wazawa ambao
wametumia gharama nafuu na kujenga miradi hiyo kwa kiwango kizuri, huku
akisisitiza wananchi wasijicheleweshee maendeleo kwa kungoja wataalamu
kutoka nje ya nchi wakati mtanzania anaweza kufanya jambo hilo kwa ubora
ule ule.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Singida Rashidi Mandoa amesema serikali kuu kupitia program ya
lipa kutokana na matokeo imetoa fedha hizo kwa ajili ya shule tatu za
Sekondari na mbili za Msingi ili kuinua ubora wa elimu Wilayani hapo.
Mandoa amesema kupitia miradi hiyo
inayotekelezwa katika sekondari za Mtinko, Ilongero na Mwanamwema Shein
pamoja na shule za Msingi za Mtinko na Mwakichenche, wananchi
wameongeza imani na matumaini makubwa kwa serikali yao.
Kwa Upande wake Kiongozi wa
Wanafunzi wa Sekondari ya Ilongero Daudi William Kihanga amesema nafasi
waliyonayo katika kumuenzi baba wa Taifa ni kusoma kwa bidii kwakuwa
wana imani kuwa kila mwalimu anapenda mwanafunzi asome kwa bidii vivyo
hivyo wakisoma kwa bidii watakuwa wanamuenzi baba wa Taifa.
Kihanga ameishukuru serikali kwa
kuboresha miundombinu ya kujifunzia kwakuwa inawapa wanafunzi hamasa ya
kusoma kwa bidii bila kikwazo chochote.
0 comments:
Post a Comment