Dkt Nchimbi ametoa agizo hilo mapema jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya ya Macho Duniani ambapo asilimia 94 ya watu wenye upofu Mkoani Singida wanasumbuliwa na matatizo ya macho ambayo yanazuilika.
Amesema ili watumishi wa umma waweze kutoa huduma iliyo bora wanatakiwa kuwa na uoni mzuri hivyo kuwapima ni hatua kubwa itakayosaidia kutibu na kuzuia upofu mapema.
“Mganga Mkuu wa Mkoa sasa tunataka uanzishe operesheni tupimwe wote macho, inasikitisha kusikia hao wote waliopata upofu takribani watu elfu 25 wangeweza kupona endapo wangegundulika mapema kwakuwa matatizo yaliyowasababishia upofu yanazuilika”, amesema Dkt Nchimbi na kusisitiza kuwa,
“Halmashauri zote tengeni bajeti za kununua dawa za macho pamoja na kuhakikisha wananchi wenu wote wanapimwa macho ili magonjwa yanayozuilika yapewe matibabu mapema, watendaji msione fahari kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa macho wakati mngeweza kuwasiadia”, ameeleza Dkt Nchimbi.
Awali, Dkt Nchimbi amepokea kifaa cha kisasa aina ya Auto Perimeter Glautefield Lite kutoka kwa Shirika la Sight Saver, chenye uwezo wa kuona taswira na matatizo ya macho vizuri, ambacho kwa nchi nzima kinapatikana mkoani Singida peke yake.
Amesema kifaa hicho kitawasaidi madaktari bingwa wa macho Mkoani hapa kutoa huduma bora huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili wapatiwe huduma kwani uwepo wa kifaa hicho bila kutumika kitakuwa hakina manufaa.
Dkt Nchimbi ameongeza kuwa, kutokunywa maji ya kutosha husababisha uoni hafifu ambao hupelekea upofu unaozuilika, hivyo amelishauri shirika la Sight Savers kuweka mpango wa kuboresha upatikanaji wa maji na kufanya utafiti hasa maofisini endapo watumishi wanakunywa maji ya kutosha kwakuwa yanasaidia kuzuia upofu.
Kwa upande wake Meneja Mipango na Uendeshaji wa Shirika la Sight Savers Nchini Mhandisi Koronel Kema amesema shirika hilo limeanzisha mradi wa kuboresha huduma za macho mkoani Singida utakaogharimu shilingi bilioni 2.8, mradi utakaodumu kwa muda wa miaka minne.
Kema amesema mradi huo utafadhili ujenzi wa kliniki za macho katika halmashauri za Iramba, Manyoni na Halmashauri ya Wilaya ya Singida na kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya ili waweze kutumia vifaa vyenye thamani ya milioni 300 ambavyo vimetolewa na shirika hilo.
Ameongeza kuwa Mkoa wa Singida umeongezewa mradi mwingine utakao anza mapema mwakani na kuhusisha upimaji wa wananfunzi wote na walimu wao mashuleni ili kuweza kutibu na kuzuia upofu katika hatua za awali.
Mmoja wa wagonjwa Said Mwiru aliyefanyiwa upasuaji katika jicho lake kwenye maadhimisho hayo amemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa kabla ya upasuaji huo hakuweza kuona chochote ila siku moja baada ya matibabu hayo anaweza kuona vizuri.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Salum Manyatta amesema ataongeza kasi katika kutekeleza agizo la mkuu wa Mkoa kwakuwa walikua tayari wameshaanza kuwapima watumishi katika baadhi ya halmashauri.
Manyatta amesema zoezi lililofanyika la upimaji watumishi katika halmashauri ya Wilaya ya Manyoni limebainisha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya watumishi hao walikuwa na matatizo ya macho ambayo yangepelekea upofu.
Katika kuadhimisha siku ya afya ya macho duniani, shirika la Sight Savers limeendesha zoezi la upimaji wa macho kwa watu 200 Mkoani hapa ambapo 84 kati yao wamegundulika kuwa na tatizo la macho linalosababisha wapoteze uwezo wa kuona, huku Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ikiwa ni ‘Afya ya Macho kwa wote’.
0 comments:
Post a Comment