METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, October 7, 2017

Madalali wa bima wapigwa ‘stop’

MENEJA WA MAMLAKA YA USIMAMIZI WA BIMA NCHINI (TIRA), STELLA LUTAGUZA.

SERIKALI imepiga marufuku madalali kupokea fedha za wateja wa mashirika ya bima mbalimbali nchini, ili kuepusha malalamiko ya kutapeliwa.

Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA), Stella Lutaguza, alisema hayo wakati wa mkutano wa kujadili mikakati ya kukabiliana na uhamiaji wa makao makuu mkoani.

Amepiga marufuku kwa wakala wa bima kutumia madalali kumletea wateja, badala yake wafuate sheria.
Alifafanua kuwa TIRA haipendi malalamiko ya wananchi kutapeliwa na madalali wa bima.

“Naomba watu wa bima wafuate sheria hiyo ya kutotumia madalali bila ya kufanya hivyo faini nyingi zitawahusu,” alisema Stella.

Alisema wanatarajia kuanza kutoa elimu kwa wakazi wa maeneo mbalimbali kuhusu umuhimu wa bima, ili watu waweze kukata bima zao za magari, afya na nyingine ambazo zinaweza kuwasaidia kipindi wanapata majanga.

Alisema pamoja na changamoto wanazopata, lakini wanatakiwa kutoka kwenda vijijini kutoa huduma hiyo kwa jamii.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Dodoma, Yasinta Mboneno, akifungua mkutano huo alisema mawakala wa bima wanatakiwa kwenda na kasi ya awamu ya tano ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

Aliwataka kuwa mstari wa mbele kuboresha huduma zao na kuacha tabia ya kuwazungusha wananchi haki zao.

Mhasibu wa TIRA Kanda ya Kati, Rogers Msagati, aliwataka mawakala kufanya kazi kwa weledi ili kuepuka usumbufu unaojitokeza kwa wateja.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com