Mwakilishi wa Shirika la Afya
Duniani (WHO) Zanzibar Dkt Ghirmay Andemichael akitoa maelezo ya Shirika
hilo kwenye warsha ya siku tatu ya kuimarisha kanuni za kupambana na
matumizi ya tumbaku inayofanyika Hoteli ya Golden Tulip Malindi Mjini
Zanzibar.
Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya
Dkt. Jamala Adam Taib akifungua warsha ya kuimarisha kanuni za
mapambano ya matumizi ya bidhaa zinazotokana na tumbaku katika Hoteli ya
Golden Tulip Malindi Mjini Zanzibar
Dkt. William Maina kutoka WHOAFRO
akitoa maelezo ya Azimio la WHO na sheria za kimataifa dhidi ya
mapambano ya matumizi ya bidhaa zinazotokana na tumbaku katika warsha ya
kuimarisha kanuni za mapambano hayo katika Hoteli ya Golden Tulip
Malindi.
Baadhi ya washiriki wa warsha ya
kumiarisha mikakati ya kanuni za kupiga vita matumizi ya tumbaku
inayofanyika Hoteli ya GoldenTulip Malindi Mjini Zanzibar.
Picha ya pamoja ya mgeni rasmi na
washiriki wa warsha ya kuimarisha mikakati ya kupiga vita matumizi ya
tumbaku inayofanyika Hoteli ya Goden Tulip Malindi Mjini Zanzibar.
Picha na Makame Mshenga.
…………………
Na Ramadhani Ali – Maelezo
Wizara ya Afya Zanzibar inaendelea
kuimarisha kanuni za kupunguza matumizi ya tumbaku baada ya kuundwa
sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2012 na kuridhia Azimio la Shirika la
Afya ulimwenguni (WHO) kupiga vita bidhaa zinazotokana na tumbaku katika
kunusuru afya za wananchi.
Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya
Dkt. Jamala Adam Taib amesema Wizara hiyo tayari imeweka kanuni ya
kukataza kuvuta sigara kwenye mikusanyiko ya watu katika kuwanusuru
waathirika wa moshi wa sigara bila ya kuwa wavutaji.
Dkt. Jamala ameeleza hayo
alipokuwa akifungua warsha ya siku tatu ya kuimarisha kanuni za
kupambana na matumizi ya tumbaku katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo
Malindi iliyowashirikisha wadau kutoka taasisi mbali mbali za Serikali.
Mkurugenzi Mkuu alisema uvutaji wa
sigara umeonekana kuwa chanzo kikubwa cha ongezeko la maradhi
yasiyoambukiza ikiwemo saratani, sukari maradhi ya mapafu na maradhi ya
ini.
Alisema pamoja na kwamba Zanzibar
haizalishi tumbaku na haina viwanda vinavyohusika na bidhaa za tumbaku
bado wananchi wamekuwa waathirika wa moshi wa sigara.
Alieleza kuwa tafiti zilizofanyika
zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya watu wanaofariki kutokana na maradhi
hayo yanatokana na kuvuta sigara ambapo asilimia 15 ya vifo hivyo
vinawafika watu wanaovutishwa moshi na wavutaji wa sigara bila ya wao
kushiriki kuvuta.
Katika kufanikisha lengo hilo
Dkt. Jamala alizishauri taasisi za Serikali, Jumuiya za kiraia na jamii
kwa jumla kuunga mkono kanuni inayokataza sigara kuvutwa kwenye
mikusanyiko ya watu na nyengine zinazoundwa ili kulinda afya zao.
Mwakilishi wa WHO Zanzibar Dkt.
Ghirmay Andemichael alisema Zaidi ya watu milioni saba wanapoteza maisha
kila mwaka duniani kutokana na matumizi ya bidhaa zinazotokana na
tumbaku ambapo asilimia 80 ya vifo vinatokea katika mataifa
yanayoendelea.
Aliongeza kuwa katika Bara la
Afrika kiasi ya watu 146,000 wenye umri kuanzia miaka 30 wanakufa kila
mwaka kutokana na maradhi yanayotokana na matumizi ya tumbaku.
Amekumbusha kuwa iwapo hatua
madhubuti hazitachukuliwa za kuandaa mikakati ya kupunguza matumizi ya
bidhaa za tumbaku nusu ya watumiaji wa bidhaa hizo watafariki kwani
tumbaku ni hatari kwa kila mtu na inatabia ya kuuwa kimya kimya.
Aliishauri Serikali, jamii na
washirika wa maendeleo kufanya juhudi za ziada kuhakikisha kanuni
zinazokaataza matumizi ya tumbaku Zanzibar zinaimarishwa na
zinatekelezwa kikamilifu.
Aliahidi kuwa WHO itandelea kutoa
kila msaada katika kuimarisha kanuni hizo ili kuiwezesha Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kufikia lengo la maendeleo endelevu la kupunguza
vifo vinavyotokana na maradhi yasiyoambukiza kwa asilimia 3.4 ifikapo
mwaka 2030.
Akizungumzia Azimio la WHO na
mikakati ya kimataifa katika mapambano ya matumizi ya tumbaku, Dkt.
William Maina alisema nchi zinapaswa kuongeza kodi ya bidhaa za tumbaku
kwa lengo la kuzipandisha bei ili baadhi ya watu washindwe kuzitumia.
Alizitaja njia nyengine kuwa ni
kupunguza matangazo ya bidhaa hizo katika vyombo vya habari, kuweka
ilani ya madhara ya tumbaku katika paketi za sigara na nchi jirani
kushirikiana pamoja katika mapambano ya matumizi ya tumbaku.
0 comments:
Post a Comment