METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, September 28, 2017

WATOA RUSHWA KATIKA UCHAGUZI WA CCM KUKIONA CHA MOTO

Kanuni ya Uchaguzi fungu la 35 (1) inaeleza bayana kwamba USHINDI wa yule ambaye ameshinda kwa vitendo vya Rushwa; kutumia au ushawishi wa Rushwa, utanyang'anywa. Aidha  Uchaguzi utafutwa na utarejewa tena na mtu anaweza kupewa adhabu ya kutoshiriki tena kwenye chaguzi za Chama. Kadharika mtu huyu anaweza kupewa adhabu kwa Mujibu wa kanuni za CCM Uongozi na Maadili; anaweza kupewa onyo kali, kama imekithiri madhira ambayo amefanya, anaweza kupewa onyo kali zaidi hata kufukuzwa Uanachama.

Hayo yalisemwa na Ndg. Humphrey Polepole Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM Taifa alipokuwa akifafanua msingi wa mfumo mzima wa CCM katika kudhibiti suala la Rushwa wakati wa uchaguzi. Akiendelea na mahojiano hayo  yaliyofanyika katika kituo cha TBC Taifa katika Taarifa ya Habari saa 2:00 usiku tarehe 28/09/2017 Ndg. Polepole alisema;

Ni haki ya kila mtanzania kujiunga na Chama chochote anachokitaka. Haki hii inakwenda sambamba na haki ya kuondoka kwenye Chama chochote ambacho alikuwa mwanachama. Imekuwepo desturi hasa kutoka Vyama Vya Upinzani kwamba ni HALALI kwa mwanachama wa CCM kuhamia Upinzani lakini ni HARAMU kwa mwanachama wa Upinzani kwenda CCM, jambo ambalo linaashiri ukosefu wa SIASA SAFI. watu wanauhuru wa kuamua wakati gani wanakaa kwenye Chama na wakati gani wanaondoka kulingana na misingi ambayo vyama hivyo imejiwekea, alisema.

Kazi kubwa anayoifanya Mhe Rais Dkt John Joseph Pombe Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM imewapa hamasa kubwa wananchi wengi wakiwemo wafuasi na wanachama wa Vyama Vya Upinzani. Kwa kufanya hivyo wengi wameamua kutoka hadharani na kumuunga mkono na wengine kuachana na Vyama vyao na kuhamia Chama Cha Mapinduzi ambacho ndicho kinampa Uongozi wa kiitikadi kiongozi huyo. Lazima tuheshimu UHURU wa watu hawa alisema.

Hivi karibuni Chama Cha Mapinduzi kiliwaomba baadhi ya viongozi wa upinzani walioibuka na tuhuma za Rushwa dhidi ya wanachama waliohamia CCM kuweka ushahidi wao hadharani, ili kama kuna wana CCM ambao pia walihusika wachukuliwe hatua kwa kuzingatia kuwa CCM inapiga vita rushwa si tu nje bali hata ndani. Kwa bahati mbaya viongozi hawa wameshindwa kujitokeza  mpaka leo jambo ambalo linaashiria kuwa ni SIASA ZA MAJITAKA.

Akijibu hoja zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Katibu Mkuu wa CCM kutohudhuria Kikao Cha Kamati Kuu, Ndg. Polepole alisema; Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa katika kikao chake kilichoanza jana 27/09/2017 kilipata taarifa rasmi ambayo ilikuja kupitia Mwenyekiti wake kuwa Kiongozi huyo ameomba udhuru wa KIHALI ambao ulikuwa unadharura ya kihali na KIUTU. Hata hivyo kabla ya udhuru huo kumpata, kiongozi huyo alishiriki kazi zote za maadalizi ya Vikao, alisema. Aidha Ndg. Polepole alitumia nafasi hiyo kuwasihi wale wote ambao wamekuwa wakilisukuma jambo hili kwenye mitandao ya kijamii hususani wafuasi, wanachama na viongozi wa upinzani kuacha KUWASHWAWASHWA na mambo ya CCM.

Akikumbushia kazi ya Vikao vya Uongozi vya Taifa, Ndg. Polepole alisema; Vikao vya Uongozi vya Taifa katika CCM vinakazi kubwa moja pamoja na mambo mengine madogo madogo; kujadili, kupitisha na kufanya uteuzi wa mwisho wa wana CCM wanaoomba ridhaa ya nafasi ya Uenyekiti wa Wilaya.

Mwisho, Ndg. Polepole alitoa wito kwa watanzania kuwa pamoja, kushikamana na kuunga mkono jitihada za Serikali za kuvunja misingi na mizizi ya kidhalimu ambayo ilikuwa ni ya kinyonyaji kwa watu masikini na wanyonge. Aidha Ndg. Polepole aliwashukuru watanzania kwa kuichagua CCM huku akitilia mkazo nia ya dhati ya CCM ya kulirudisha Taifa kwenye misingi yake ya kushugulika na shida za watu.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com