Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amekutana na Balozi wa Iran. Mousa Farhang nakufanya mazungumzo ya
kikazi leo Septemba 13/2017.Ofisini kwake Magogoni Dar es salaam. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Tanzania ipo salama na imara na kwamba mtu yeyote atakayejaribu
kutaka kuvuruga amani atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano,
Septemba 13, 2017) alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Iran
nchini Tanzania, Bw. Mousa Farhang jijini Dar es Salaam.
“Hatua kali zitachukuliwa kwa
yeyote kutoka popote atakayejaribu kuvuruga amani yetu. Nawaomba
wananchi muwe makini na muendelee kuidumisha amani yetu.”
Amesema kwa sasa Serikali ipo
katika mapambano dhidi ya vitendo vya ufisadi, rushwa, biashara haramu
ya dawa za kulevya pamoja na wahujumu uchumi.
Waziri Mkuu amesema licha ya
Tanzania kuwa ni nchi ya amani na yenye utulivu wa kisiasa, wameendelea
kuwahamasisha wananchi wake kudumisha mshikamano.
Amesema mbali ya kuimarisha amani
nchini, pia Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji jambo ambalo
litawawezesha watakaokuja kuwekeza nchini kupata tija.
Hivyo ametumia fursa hiyo
kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini Iran ili waje kuwekeza kwenye
viwanda mbalimbali vikiwemo vya kuchakata mazao ya kilimo.
Pia amewakaribisha raia wa Iran
kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyoko nchini Tanzania kama
mlima wa Kilimanjaro, fukwe, mali kale na mbuga za wanyama.
Kwa upande wake, Balozi Farhang
ameipongeza Serikali kwa kuwa na dhamira ya dhati ya kuimarisha uchumi
na kupambana na dawa za kulevya na ufisadi.
Balozi huyo amesema Serikali ya
Irani ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika mapambano
dhidi ya rushwa, ufisadi pamoja na vitendo vingine vya kihalifu.
Balozi Farhang ametumia fursa hiyo
kuiomba Serikali ya Tanzania ifungue Ofisi ya Ubalozi nchini Iran ili
kuimarisha uhusiano huo, ambapo Waziri Mkuu amekubali.
Pia Bw. Farhang amesema aliwahi
kutembelea mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro na kusema kwamba
ni maeneo mazuri ambayo hajawahi kuyaona tangu azaliwe.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, SEPTEMBA 13, 2017.
0 comments:
Post a Comment