METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, September 26, 2017

SPANEST YASIFU MAONESHO YA UTALII YA KARIBU KUSINI


ZAIDI ya wajasiriamali 350 wamejitokeza kushiriki maonesho ya utalii ya Karibu Kusini yanayoanza mjini Iringa kesho Septemba 27 hadi Oktoba 2 katika viwanja vya Kichangani mjini Iringa.

Maonesho hayo yameandaliwa na mikoa ya nyanda za juu kusini kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii,  shirika la kuhudumia viwanda vidogo (Sido) na wadau mbalimbali ukiwemo Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST).

Akizungumza na wanahabari jana, Mratibu wa Spanest, Godwell Ole Meing’ataki alisema ushiriki wa wadau hao ni mafanikio makubwa katika sekta ya utalii inayoanza kutumiwa na wajasiriamali hao kutangaza bidhaa zao.

“Watu wa kusini wana fursa kubwa sana ya kuongeza mapato yao kwa kupitia sekta hii ya utalii. Mikoa ya kusini ina rasilimali na vivutio vingi, vikihifadhiwa na kulindwa vitaleta wageni wengi na hivyo kuchochea shughuli zingine za maendeleo,” alisema.

Meing’ataki alisema maonesho ya mwaka huu yamekuwa bora zaidi kwasababu kamati inayoyaratibu imejitahidi kwa kiwango kikubwa kushughulikia changamoto mbalimbali zilizojitokeza mwaka jana wakati yakifanyika kwa mara ya kwanza.

“Kwa Spanest haya ni mafanikio makubwa na ni matokeo ya mradi wetu kusaidia kuwaleta wadau mbalimbali wa uhifadhi na utalii ili waweze kwa pamoja kushughulikia changamoto mbalimbali katika maeneo hayo,” alisema.

Katika uhifadhi, Meing’ataki alisema SPANEST inayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) imefanya mengi yakiwemo mafunzo kwa askari wanyamapori na imetoa vifaa mbalimbali vinavyosaidia kuboresha na kukabiliana na ujangili ndani na nje ya maeneo yaliyohifadhiwa.

“Na kwa upande wa utalii tumekuwa tukiwapeleka wadau katika maonesho ya Karibu Fair ya Arusha ili kujifunza na kutumia fursa hiyo kutangaza utalii na shughuli za ujasiriamali zinazofanywa kusini,” alisema.

Katika kuboresha huduma za hoteli, alisema Spanest imetoa mafunzo kwa watoa huduma na imeshiriki pia kuandaa mipango mikakati ya kuendeleza utalii katika mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya.

Meing’ataki alisema maonesho ya utalii ya Karibu Kusini yanaweza kuwa maonesho ya utalii ya kimataifa kwa kadri yanavyozidi kukua na kwa kuzingatia fursa za kiuchumi na utalii zilizoko katika mikoa hiyo.

Alisema kukua kwa sekta hiyo ya utalii kunapaswa pia kwenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege, mfumo mzima wa mawasiliano na vituo vya kutolea taarifa na kuhakikisha huduma za hoteli na waongoza watalii zinaimarishwa ili kukidhi viwango vinavyotakiwa.

“Tunataka kuona miaka kadhaa ijayo maonesho haya na vivutio vya utalii katika mikoa ya kusini vinaleta wageni wengi zaidi na hilo likifanikiwa litasaidia kunyanyua shughuli za wajasiriamali na mapato ya wakazi wa mikoa hiyo na hivyo kuhifurahi sekta hiyo,” alisema.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com