Ahimiza nyumba za ibada zisitumiwe vibaya
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaomba
waumini wa dini za Kiislamu na Kikristo nchini wahakikishe nyumba zao za
ibada hazitumiki kuleta migogoro.
Ametoa ombi hilo jana usiku (Jumatano,
Juni 21, 2017) wakati akizungumza na mamia ya waumini wa dini za
Kikristo na Kiislamu pamoja na viongozi wa dini walioshiriki ibada ya
futari wilayani Chato, mkoani Geita.
Akizungumza na waumini hao kwa niaba ya
Mheshimiwa Rais, Dk. John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu alisema Mheshimiwa
Rais alishapanga kufika Chato ili kushiriki nao ibada ya iftar lakini
ametingwa na majukumu ya kitaifa akaona ni vema amtume yeye ili
amwakilishe.
“Mheshimiwa Rais alishapanga kuja Chato
kufuturu pamoja na wana-Chato lakini kadri siku zinavyozidi kwenda
anajikuta anabanwa na majukumu mengi ikiwemo kukutana na wageni wa
kimataifa, kwa hiyo akaona ni vema nije kumwakilisha katika shughuli
hii,” alisema.
“Mheshimiwa Rais anawaombea heri katika
siku zilizobakia za mfungo wa Ramadhan ili mmalize salama na Mungu
akijalia muweze kusherehekea pamoja, na pia anawatakia heri wale
watakaoendelea na sita tushawal.”
Akisisitiza kuhusu amani na utulivu
nchini, Waziri Mkuu alisema: “Hatupendi kusikia kuwa msikiti fulani
wamechapana viboko kwa sababu ya kugombea uongozi au kwenye kanisa
fulani waumini wamepigana wakigombea mchungaji wao.”
“Tutumie nyumba zetu za ibada kudumisha
amani na mshikamano wetu. Napenda niwahakikishie kuwa Serikali yenu
chini ya Rais John Pombe Magufuli itaendelea kuheshimu dini zote.”
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo
kuwakumbusha waumini hao kwamba mwezi mtukufu wa Ramadhan ni wa toba kwa
kila muumini. “Huu mwezi mafundisho yake yanasisitiza amani, uvumilivu
na kusameheana. Nipende kuwasihi kwamba tuendelee kudumisha utulivu
tulionao,” aliongeza.
“Nipende kusisitiza kwenu wana-Geita na
wana-Chato kwamba jukumu kubwa mlilonalo ni kuendelea kumuombea
Mheshimiwa Rais ili Mwenyezi Mungu amjalie afya njema, busara na uongozi
wa kimungu katika maamuzi yake. Niwasihi ndugu zangu Waislamu na
Wakristo, tuendelee kuwaombea viongozi wote wa kitaifa kila siku ili
wafanye kazi kwa kuongozwa na Mungu,” alisema.
Awali, akisoma risala mbele ya Waziri
Mkuu, Katibu wa BAKWATA Wilaya ya Chato, Sheikh Ally Moto alisema
wanamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapa fursa ya kuweza kushiriki ibada
ya iftar pamoja na watoto yatima na wajane.
Alisema wanaunga mkono jitihada
zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano na ili kudumisha amani
wilayani humo, waumini wa Kiislamu na Kikisto wameunda Kamati ya Amani
ya wilaya hiyo inayojulikana kama Interfaith Committee.
Naye Mbunge wa Chato ambaye pia ni Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani alisema anamshukuru
Mheshimiwa Rais kwa kuandaa futari hiyo ambayo imejumuisha wana Chato
kutoka pembe nne za wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa
Kamati ya Amani ya Mkoa wa Geita, Askofu Mussa Magwesera wa Kanisa la
African Inland Church (AIC), Dayosisi ya Geita alitoa shukrani kwa
Mheshimiwa Rais Magufuli na kuwapongeza viongozi wakuu wa kitaifa
kutokana na utendaji wao unaogusa mioyo ya Watanzania.
“Ninyi wote watatu ni viongozi ambao
Mungu amewaweka kuongoza nchi yetu. Katika miezi hii 18, mmefanya mambo
makubwa, ni imani yetu kuwa ataendelea kuwaongoza katika utendaji kazi
wenu,” alisema.
Akitoa shukrani, Sheikh wa Mkoa wa
Geita, Sheikh Yusuph Kabaju ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya
Amani ya Mkoa huo, alimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuwapa fursa
wana-Geita kujumuika pamoja katika futari hiyo na kuahidi kudumisha
amani ya Tanzania.
“Tunakushukuru kwa kutuunganisha wana
Geita katika futari hii japo umeamua kufanyia ibada hii hapa Chato.
Maneno ya Quran tukufu yanasema malipo ya waliofunga anayapata pia yule
aliyefuturisha waliofunga,” alisema.
Sheikh Kabaju pia alisoma dua ya
kumuombea Mheshimiwa Rais Magufuli pamoja na viongozi wa kitaifa. Pia
aliombea amani kwa ajili ya Taifa la Tanzania.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, JUNI 22, 2017.
0 comments:
Post a Comment