METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, September 1, 2017

DC MTATURU AWATAKA WANANCHI KULINDA AMANI NA UTULIVU NCHINI

Na Mathias Canal, Singida

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida Mhe Miraji Jumanne Mtaturu amesema kuwa Mafunzo ya dini na imani za dini zina imarisha Umoja na Mshikamano kwani inawafanya Wananchi kuwa raia wema na kusameheana pale wanapokeseana.

Dc Mtaturu Ameyasema hayo leo Septemba 1, 2017 Wakati alipoungana na waislamu kuswali Swala ya EID EL HAJJI katika Kijiji cha Mang'onyi Wilayani humo.

Alisema serikali ina amini kuwa waumini wakifuata miongozo na taratibu za dini itakuwa Ni njia sahihi ya kujenga Upendo na Mshikamano ambao ndio silaha ya mafanikio na uimara wa nchi katika kuleta maendeleo nchini.

Alisema kuwa waumini wa dini zote nchini wanapaswa kuendelea kulinda amani na Mshikamano uliopo nchini pasina kubagua dini wala kabila kwani amani ndio msingi wa kila kitu pasina  amani hata ibada hazitaweza kufanyika.

DC Mtaturu Alisema kuwa wananchi wanatakiwa kuwa wamoja kama nchi na kuachana na wanasiasa wanaopotosha Umma na kuwagombanisha Wananchi na Serikali yao.

Huku akieleza kuwa vyama vya siasa vinapaswa kuwa chachu ya Maendeleo katika Jamii kwani siasa sio uadui na vyama ni kuonyesha tu Demokrasia na njia ya kufikisha maendeleo kwa Wananchi.

Mhe Mtaturu Alisema kila unapomalizika  Uchaguzi Mkuu Viongozi wa vyama vya siasa kwa kushirikiana na Wananchi kwa ujumla wanapaswa kuwa chachu ya kusukuma maendeleo Endelevu.

"Hapa katikati tumeshuhudia baadhi ya wanasiasa kuwa na kauli za kuwagawa wananchi na kuwachonganisha na serikali yao jambo hili Ni baya Sana tena linadhoofisha maendeleo" Alisema Mtaturu

Aliwataka wanasiasa kuacha siasa zinazokwamisha maendeleo vinginevyo itatafsiriwa ni ulimbukeni wa siasa kwani walioanzisha siasa za vyama vingi wengine wana zaidi ya miaka 200 ila wakimaliza uchaguzi jioni wakiamka asubuhi siasa zinaisha wanafanya maendeleo na kuwaunganisha wananchi.

Hata hivyo Mhe Mtaturu amewahamasisha Wakulima Wilayani  Ikungi kulima mazao yanayotosheleza kwa chakula huku akisema kuwa serikali imekuja na zao la korosho na msimu huu Wananchi watapewa mgao wa miche 500,000 bure.

Kwa upande wake mjumbe wa Halmashauri kuu ya BAKWATA Wilaya ya Ikungi Sheikh Salum Ngaa alieleza maudhui ya siku ya Idd El Haji ni waumini  kufanya yale wanayofanya mahujaji walipo Hijja hivi leo, kwani Hijja ni miongoni mwa nguzo za Dini ya Kiislamu huku akimpongeza Mkuu huyo wa Wilaya ya Ikungi kwa kujumuika na Wananchi kusali pamoja sala ya Eid El Hajji.

Aidha, Mhe Mtaturu alichangia Bando  moja ya Bati ambayo Ni sawa na bati16, mifuko 10 ya Saruji kwa ajili ya ujenzi wa madrasa ya vijana watakayojifunzia dini kwani wapo kwenye hatua ya upauaji.

Pia waumini wengine waliunga mkono juhudi hizo za ujenzi kwa kuchangia  fedha taslimu Tsh 327,950 ambapo Kati ya fedha hizo ahadi Ni Tsh 30,000 mifuko 7 ya Saruji na bati 14.

MWISHO.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com