METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, August 20, 2017

ZAIDI YA MILIONI 2.9 ZAKUSANYWA KUTUNISHA MFUKO WA ELIMU WILAYANI IKUNGI

Na Mathias Canal, Singida

Zaidi ya shilingi milioni 2.9 zimekusanywa kwa ajili ya kutunisha mfuko wa elimu Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida ili kuboresha changamoto katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuboresha nyumba za walimu, Maabara ya masomo ya sayansi kwa shule za sekondari, Madarasa kwa shule za msingi, Samani za shule (meza na viti kwa shule za sekondari) pamoja na vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

Katika harambee ya papo hapo iliyoendeshwa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu wadau wa elimu na wananchi kwa ujumla walioshiriki katika uzinduzi wa zoezi la ufyatuaji matofali kwa ajili ya kuanza ujenzi wa miundombinu hiyo, ilipatikana zaidi ya milioni mbili laki tisa (2,900,000)  Fedha taslimu ikiwa ni shilingi 805,000 na ahadi ikiwa ni shilingi milioni moja na laki tisa (1,200,000).

Mhe Mtaturu alichangia mifuko 100 ya saruji yenye thamani ya shilingi milioni 1,350,000 huku wadau wengine wakichangia mifuko 194 ya saruji yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni mbili na laki sita.

Akisoma taarifa ya uzinduzi wa "Ikungi Elimu Cup Mwaka 2017" mbele ya mgeni rasmi katika Ufunguzi Wa Mashindano ya Hayo ambaye ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt Angeline Lutambi aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe Dkt Rehema Nchimbi pamoja na wananchi na wadau wa elimu Wilayani humo sherehe zilizofanyika katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Ikungi, Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Miraji Jumanne Mtaturu alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa Wilaya hiyo na kuanza kuwatumikia wananchi wake Mwezi Julai Mwaka 2013 kumekuwa na upungufu wa nyumba 628 za walimu kwani zilizopo ni nyumba 387 pekee ikiwa ni sawa na upungufu wa asilimia 61.87% jambo ambalo linarudisha nyuma hamasa ya walimu katika ufundishaji.

Hivyo ili kukabiliana na kadhia hiyo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya imeanzisha Akaunti maalumu itakayotumiwa na wadau wa elimu na wananchi kwa ujumla kuchangia kiasi cha fedha kwa kadiri ya uwezo wao ili kuboresha miundombinu ya waalimu sambamba na changamoto zingine zinazoikabili sekta ya  elimu ambazo ni pamoja na upungufu wa Vyumba vya madarasa 595 kwani yaliyopo ni madarasa 387 ambapo uhitaji ni madarasa 1,315.

Alieleza pia upungufu mkubwa upande wa Maabara za sayansi kwani zilizopo ni maabara 4 pekee kati ya maabara 90 zinazohitajika hivyo kupelekea kuwa na upungufu wa maabara 86.

Alisema kuwa kamati kuu tendaji ya Mfuko wa Elimu wilaya ya Ikungi imeandaa mpango mkakati wa miaka mitatu kuanzia Julai 2017 hadi June 2020 ambapo lengo kuu la mkakati wa mfuko wa elimu ni kushirikisha wadau mbalimbali wa elimu wakiwemo wananchi, Mashirika, Taasisi, Makampuni ya ndani na nje ya nchi katika kutafuta Rasilimali fedha.

Katika Mpango mkakati huo zinahitajika jumla ya shilingi 3,000,077,500/= (Elimu ya Msingi Shilingi 1,605,250,000/=  na Elimu ya Sekondari Shilingi 1,394,827,500/=) ili kuweza kutatua baadhi ya changamoto hizo.

Alisema kuwa katika ufyatuaji wa matofali nguvu za wananchi zitatumika pia wananchi watajitolea vifaa kama maji, Mashine Vibao na Mchanga.

Aidha, Mhe Mtaturu amewashukuru wadau wa Elimu na Wananchi kwa ujumla wake kwa kushiriki katika Ufunguzi Wa Mashindano hayo na kukubali kwa kauli moja kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli katika kuimarisha na kuboresha MAISHA ya watanzania.

MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com