Katibu Tawala wa Wilaya ya
Longido mkoani Arusha, Bw. Toba Nguvila (kushoto), akimweleza jambo
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB, Kanda ya
Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro (katikati) kabla ya kutembelea
Soko la Kisasa Mifugo linalojengwa katika kijiji cha Worendeke, kata ya
Kimokouwa, wilayani Longido, mkoani Arusha, linalojengwa kutokana na
mkopo wenye masharti nafuu wa sh. Milioni 650 kutoka Benki hiyo. Kulia
ni Afisa anayeshughulikia Dawati la Beni ya Maendeleo ya Afrika-AfDB
kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Said Nyenge.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika-AfDB, kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje
Weggoro akisikiliza maelezo ya mradi wa ujenzi wa Soko la Kisasa la
Mifugo katika kijiji cha Worendeke, kata ya Kimokouwa, wilayani Longido
mkoani Arusha, unaogharimu shilingi milioni 650, ikiwa ni mkopo wenye
masharti nafuu kutoka Benki hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika-AfDB, Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje
Weggoro, akisisitiza jambo baada ya kusikiliza maelezo ya mradi huo wa
Soko la Kisasa la Mifugo linalojengwa katika kijiji cha Worendeke, kata
ya Kimokouwa wilayani Longido mkoani Arusha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
Maendeleo ya Afrika-AfDB, kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje
Weggoro (wapili kulia) akimweleza jambo Katibu Tawala wa wilaya ya
Longido mkoani Arusha, Bw. Toba Nguvila, wakati Mkurugenzi huyo
alipotembelea na kukagua ujenzi wa Soko la Kisasa la Mifugo,
linalojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 650 kupitia mkopo nafuu wa
Benki hiyo kwa Serikali ya Tanzania.
Baadhi ya wafugaji wa kijiji cha
Worendeke, kata ya Kimokouwa, wilayani Longido mkoani Arusha,
wanaonufaika na uwepo wa soko hilo ambapo wameanza kuuza mifugo yao kwa
faida kubwa badala ya kupeleka mifugo yao nchi jirani ya Kenya ambako
walikuwa wakipata adha kubwa na faida ndogo kutokana na gharama kubwa
walizokuwa wakitumia kufikisha mifugo yao nchini humo.
(Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
Benny Mwaipaja, WFM, LONGIDO-ARUSHA
WAFUGAJI wilayani Longido Mkoani
Arusha wameanza kunufaika na ujenzi wa soko la kisasa la mifugo
linalojengwa na Serikali katika kijiji cha Worendeke kata ya Kimokouwa,
kupitia mkopo wa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB
Baadhi ya wafugaji wamesema kuwa
Soko hilo linalojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 650,
limewaondolea adha kubwa waliyokuwa wakiipata walipokuwa wakiuza mifugo
yao nchini Kenya kutokana na gharama kubwa ya kusafirisha mifugo kwenda
huko pamoja na kulipa kodi na ushuru mbalimbali.
Wamesema kuwa kujengwa kwa somo
hilo ni mkombozi mkubwa kwao na kwamba hali hiyo itasisimua uchumi wao
kwa kuwa wafanyabiashara wa ndani na kutoka Kenya wamekuwa wakiwafuata
kwenye soko hilo kununua mifugo yao hatua inayowafanya wapate faida
kubwa.
Katibu Tawala wa Wilaya ya
Longido, Bw. Toba Nguvila, amesema kuwa soko hilo ambalo ujenzi wa
miundombinu yake umekamilika kwa asilimia 85 limeanza kuiingiza Serikali
mapato yake ambapo kwa wastani Halmashauri ya wilaya inakusanya wastani
wa shilingi milioni 1 kwa siku.
“Asilimia 95 ya wakazi wa wilaya
yetu ni wafugaji wa kimaasai ambao kwa kipindi kirefu wameteseka
kusafirisha mifugo yao kwenda Kenya na kutopata faida kutokana na
gharama kubwa ya kusafirisha, kupitisha mifugo kwenye maeneo ya watu
hivyo kulazimika kulipa ushuru, halikadhalika kulipia tozo mbalimbali
wakati wakisubiri kuuza mifugo yao” alieleza Bw. Nguvila
Alisema kuwa kuanzishwa kwa soko
hilo litakalokuwa na miundombinu muhimu kama vile mizani ya kupimia
uzito wa mifugo yao kabla ya kuiuza, si tu kwamba limesababisha wafugaji
kupata faida kwa kuuza mifugo yao kwa bei nzuri ya soko, bali pia
limeleta neema kwa wafanyabiashara wengine wadogo wakiwemo mamalishe.
“Akina mama wanafanyabiashara zao
za kuuza chai na chakula huku kundi kubwa la vijana waliokuwa wakiuza
bidhaa zao za kutembeza mikononi katika mpaka wa Kenya na
Tanzania-Namanga, ambao wamejiajiri kwa shughuli za kushusha na kupakia
mifugo kwenye malori” aliongeza Bw. Nguvila
Alisema kuwa katika kuhakikisha
kuwa mifugo inaongezewa thamani, mchakato wa kuanzisha kiwanda
kikubwa cha kuchakata nyama kitakachokuwa na uwezo wa kuchakata mifugo
3,000 kwa siku kinatarajiwa kujengwa katika eneo la karibu na soko hilo
kwa ajili ya kuuza nyama ndani na nje ya nchi
“Taratibu za kuanzishwa kwa
kiwanda hicho zimekamilika na wakati wowote ujenzi wake utaanza hatua
ambayo tunaamini watu wetu watanufaika zaidi na biashara ya mifugo
kuliko ilivyokuwa hapo awali ikiwa ni juhudi za Serikali ya aAwamu ya
Tano ya kuwahudumia wananchi wa hali ya chini ili kuboresha maisha yao”
alisisitiza katibu Tawala huyo
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika anayesimamia nchi 7 za Kanda ya
Afrika Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro, amesema Benki yake
imefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa soko hilo litakalochochea uchumi
wa wananchi.
Ameahidi kuwa Benki yake
inafadhili ujenzi wa masoko mengi ya namna hiyo hapa nchini na nchini
nyingine za Kiafrika ili nchi hizo ziweze kukuza uchumi wake na maisha
ya watu wake kwa ujumla.
“Benki iko tayari kuendelea
kusaidia eneo hili la ujenzi wa masoko ili kuchochea kasi ya maendeleo
ya kiuchumi hivyo naushukuru uongozi wa mkoa wa Arusha na Wilaya ya
Longido kwa kazi nzuri wanayoifanya kusimamia ujenzi wa soko hili na
kwamba ujenzi wake utakamilika kwa wakati kama ilivyopangwa”Alisisitiza
Dkt. Weggoro.
Benki ya Maendeleo ya Afrika-AfDB
inafadhili ujenzi wa masoko kadhaa Tanzania Bara na Visiwani kupitia
mkopo wenye masharti nafuu wenye thamani ya Dola za kimarekani milioni
56 na unatekelezwa kupitia mpango wa kuendeleza miundombinu ya masoko,
kuongeza thamani ya mazao na uboreshaji wa huduma za kifedha vjijini.
0 comments:
Post a Comment