Na Veronica Simba, Kagera
Serikali za Tanzania na Uganda zimetiliana saini Mkataba wa Makubaliano ya Awali (MoU) wa kupeleka umeme kwenye Vijiji vya Mpakani mwa nchi hizo.
Serikali za Tanzania na Uganda zimetiliana saini Mkataba wa Makubaliano ya Awali (MoU) wa kupeleka umeme kwenye Vijiji vya Mpakani mwa nchi hizo.
Hati
ya Makubaliano hayo ilisainiwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Mambo ya
Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dk. Augustine
Mahiga akiwakilisha Wizara ya Nishati na Madini (Tanzania) na Waziri wa
Nishati wa Uganda, Dk. Simon D’Ujanga, wakati wa Mkutano wa Mawaziri wa
nchi hizo kuhusu ushirikiano kwenye masuala ya mpakani, uliofanyika
mjini Bukoba, wilayani Kagera.
Makubaliano
ya msingi katika Hati iliyosainiwa ni utekelezaji wa Mradi wa kupeleka
umeme kwenye vijiji vya Nangoma, katika eneo lililopo mpakani mwa
Tanzania na Uganda na vijiji vingine vya maeneo hayo kwa kutokea upande
wa Tanzania.
Akifafanua
zaidi kuhusu makubaliano husika, Naibu Waziri wa Nishati na Madini,
Dkt. Medard Kalemani, ambaye pia alishiriki Mkutano huo mkubwa, alisema
kuwa Wakala wa Nishati Vijijini kwa upande wa Tanzania (REA-Tanzania)
utahusika katika kugharamia ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa
kilovoti 33 kufikisha umeme katika eneo la mpakani, umbali wa kilomita
0.8 kwa gharama ya Dola za Marekani 36,923.05.
Aidha,
aliongeza kuwa, kwa upande wa Uganda, Wakala wa Nishati Vijijini wa
nchi hiyo (REA-Uganda) utahusika kugharamia ujenzi wa njia ya umeme ya
msongo wa kilovoti 33 umbali wa kilomita 7.5 kutoka eneo la mpakani hadi
katika vijiji vya Bukwali Gamuli, Bushungulu, Nangoma, Omurushenye,
Mizinda na Lukunyu kwa gharama ya Dola za Marekani 724,239.06.
Alieleza
kuwa, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), litakuwa na jukumu la kuuza
umeme kulingana na Mkataba wa kusambaza umeme utakaosainiwa kati yake na
Shirika la Umeme la Uganda.
Vilevile,
alisema kuwa, REA-Tanzania itashiriki katika kusaidia upatikanaji wa
Mkandarasi atakayehusika na ujenzi wa Mradi kwa upande wa Uganda.
Katika
Mkutano huo pia, masuala mengine ya ushirikiano baina ya Tanzania na
Uganda, katika sekta ya nishati yalijadiliwa ambapo ilielezwa kuwa,
mwaka 2014, Serikali hizo mbili zilisaini makubaliano (Bilateral
Agreement) kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa kuzalisha umeme wa
Murongo-Kikagati wa Megawati 14 kwa manufaa ya nchi zote mbili.
Mradi
mwingine wa ushirikiano katika sekta ya nishati, uliojadiliwa katika
Mkutano huo ni wa kuzalisha umeme wa Nsongezi wa Megawati 35, ambapo
ilielezwa kuwa, Serikali za Tanzania na Uganda zina nia ya kutekeleza
Mradi huo kwa kutumia chanzo cha maji ya Mto Kagera ambao upo mpakani
mwa nchi hizo.
Wataalam
wamependekeza kuwa, hatua muhimu za utekelezaji wa miradi kama vile
kufanya Upembuzi yakinifu wa Mradi, upatikanaji wa Mshauri Mwelekezi na
Mwendelezaji wa Mradi, zifanyike kwa Ubia, chini ya uongozi wa Serikali
ya Tanzania na Uganda.
Masuala
mengine ya ushirikiano baina ya nchi za Tanzania na Uganda katika
maeneo ya Mpakani, yaliyojadiliwa katika Mkutano huo wa Mawaziri ambao
uliandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
(Tanzania) ni kilimo na uvuvi, maji, ardhi pamoja na masuala ya ulinzi
na usalama.
Mkutano
wa Mawaziri wa Tanzania na Uganda ulitanguliwa na Mkutano wa Makatibu
Wakuu wa Wizara mbalimbali kutoka nchi hizo mbili wanaoshughulika na
masuala ya ushirikiano katika maeneo ya Mpaka, uliofanyika Julai 28,
mwaka huu mjini Bukoba.
0 comments:
Post a Comment