Kufuatia
mwaliko wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Abdel Fattah Al Sisi, Rais wa
Jamhuri ya Kiarabu ya Misri atafanya Ziara ya Kitaifa nchini Tanzania
wiki ijayo. Hii itakuwa ni ziara ya kwanza ya Mheshimiwa Abdel Fattah Al
Sisi nchini Tanzania tangu Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli aingie
madarakani.
Lengo
la ziara hii ni kuimarisha na kukuza zaidi mahusiano mazuri yaliyopo ya
kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizi mbili, ziara hii
pia itatoa fursa kwa viongozi wetu kujadili masuala mbalimbali
yanayohusu nchi hizi mbili, ya kikanda na kimataifa.
Mheshimiwa
Rais Al Sisi atawasili nchini kupokelewa na mwenyeji wake, Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Aidha, Mheshimiwa Rais Al Sisi mchana atakuwa na mazungumzo
(tete-a-tete) na mwenyeji wake kabla ya kushiriki mazungumzo rasmi
(official talks) na baadae jioni Mheshimiwa Rais Al Sisi atahudhuria
dhifa ya kitaifa itakayoandaliwa na mwenyeji wake.
Tanzania
na Misri zina mahusiano mazuri ya kidiplomasia ya muda mrefu ambayo
yamezidi kuimarika hasa katika miaka ya karibuni. Ushirikiano huu
unatokana na misingi ya mahusiano na mashirikiano ya karibu sana kati ya
Marehemu Baba wa Taifa na muasisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Kiongozi mashuhuri wa Misri na
muasisi wa Jamhuri ya Taifa la Kiarabu ya Misri, Marehemu Gamal Abdel
Nasser.
Uhusiano
wa nchi hizi mbili umejengwa katika misingi ya ushirikiano na maelewano
katika Nyanja za kijamii, kiuchumi, kisiasa, kiulinzi na kiusalama
pamoja na medani za siasa za ushirikiano kimataifa, kutetea haki za
binadamu, kuimarisha umoja na maendeleo ya Afrika, ukombozi wa Bara la
Afrika na kupinga ukoloni, dhuluma na aina zote za ukandamamizaji
duniani. Uhusiano huu umejengwa katika Nyanja zote za uhusiano katika
sekta za huduma za kijamii na kiuchumi zikiwemo elimu, afya, kilimo,
mawasiliano, usafiri, ulinzi na usalama na ushirikiano wa kimataifa.
Misri
ni nchi ya pili yenye uchumi mkubwa Barani Afrika. Takwimu za mwaka
2016, zinaonesha kwamba pato la taifa (GDP) la Misri lilikuwa Dola za
Kimarekani Billioni 266.213. Sekta kubwa kabisa katika uchumi wa Misri
ni sekta ya huduma ( huduma za benki, mawasiliano, usafirishaji na
utalii) ambayo inachangia takribani asilimia 52.5 kwenye GDP. Viwanda
(manufacturing) inachangia asilimia 36.3, na kilimo asilimia 11.2.
Tanzania
na Misri zinashirikiana katika ngazi za taasisi za serikali ambazo ni
Taasisi ya Udhibiti wa utawala ya Misri (Administration Control
Authority of Egypt) ambayo inashirikiana na Taasisi ya kupambana na
kuzuia Rushwa ya Tanzania (TAKUKURU), Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na
Hospitali ya Rufaa ya Mnazi mmoja zimesaini makubaliano ya Ushirikiano
na Hospitali ya El Shatby ya Chuo Kikuu cha Alexandria nchini Misri,
Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kina mashirikiano ya
kubadilishana wataalamu na usimamizi wa pamoja wa Shahada za juu za
uzamili na uzamivu na Chuo Kikuu cha Azhar cha Misri, Jeshi la Wananchi
wa Tanzania kupitia SUMA JKT wamesaini Makubaliano ya Ushirikiano na
Kampuni ya Polyserve ya Misri .
Aidha,
kutokana na takwimu za kituo cha Uwekezaji (TIC) kimesajili jumla ya
miradi nane kati ya mwaka 1990 hadi 2017, miradi hii ina jumla ya
thamani ya Dola za Kimarekani 887.02 na kutoa ajira zipatazo 953,
uwekezaji huo ni katika maeneo ya Kilimo, viwanda(mbao, mbolea, madini,
dhahabu na shaba) na sekta ya Huduma.
Hivyo ziara hii ina umuhimu mkubwa sana hasa katika wakati huu ambapo msisitizo wa Serikali ni katika kujenga uchumi wa viwanda.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam
11 Agosti, 2017.
0 comments:
Post a Comment