METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, August 10, 2017

JOHN MWIRIGI: DARASA JIPYA KWA VIJANA WA TANZANIA

Na Francis Daudi, Bangalore
+91 9513833624.

Uchaguzi wa Kenya umemalizika na sasa ni matokeo tu ya uraisi yanasubiriwa kwa hamu.
Ila habari kubwa imekuwa ushindi wa kijana John Paul Mwirigi katika jimbo la Igembe Kusini. Mwirigi  ambaye ana umri wa miaka 23 tu, amemuangusha mgombea wa chama cha Jubilee, Bwana Rufus Miriti ambaye alifanya kampeni ya gharama kubwa zaidi.

John Mwirigi ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Mlima Kenya akisomea shahada ya Ualimu, na alipoteza wazazi wote wawili akiwa mdogo sana. Hivyo maisha yake yote ameishi kama mtoto yatima ambaye amekuwa akisaidiwa tu na watu baki, yeye ni mtoto wa sita kati ya nane kwenye familia yake.

Akiongea na gazeti la ‘The Nation’ anaeleza kuwa alianza kuwaomba marafiki wamsaidie katika kampeni akiwa kidato cha tatu kwenye shule ya sekondari Kirindine. Wakati wa kampeni za uchaguzi huu, Mwirigi hakuwa na mabango wala gari la kampeni kama wagombea wengine.

Alitembea kwa mguu toka nyumba moja mpaka ingine kuomba kura, vijana wa bodaboda waliungana nae ‘kuuza’ sera zake. Anaeleza wakati mwingine hata aliishiwa ‘salio’ la simu wakati wa kampeni. Mwirigi alisimama kama mgombea binafsi kwani hakuweza kuingia kwenye michakato ya uteuzi ndani ya vyama.

Mwirigi alichoshwa na kampeni ngumu kiasi kwamba alitaka kukata tamaa lakini alitia juhudi kila siku mpya. Ni kijana ambaye hakujuana na watu wakubwa katika siasa, pia hakuwa na pesa za kutosha. Jana matokeo yalipotangazwa ilikuwa shangwe kubwa kwani alipata kura 18, 867 na mgombea mwingine ambaye ilitarajiwa kuwa atashinda Bwana Rufus Miriti alipata kura 15, 411. Hii inamfanya John Paul Mwirigi kuwa ndiye mbunge mdogo kuliko wote katika historia ya Kenya.

John Mwirigi  ni darasa kwa  vijana wa Afrika kujituma kwa kile tunachokitaka. Anatufunza kuacha kulalamika na kusubiri kusaidiwa.  John Mwirigi  ni shamba darasa la kujifunzia kufanya kazi na kusimamia malengo yetu. Afrika na Tanzania yetu haiwezi kwenda mbele kwa kulalama na kupinga kila kitu. Tanzania haitaendelea kwa vijana wasiofanya kazi na kushinda kujadili mambo ambayo  kimsingi hayatalisukuma Taifa letu mbele.

Wapiga kura wa  jimbo la Igembe kusini wanasema walimpa kura John Mwirigi  kwani ni kijana mwadilifu na ambaye hakukubali kuwekwa ‘mfukoni’ na wanasiasa  walaghai. Pia alipendwa zaidi kwani anajua matatizo ya wananchi wa kawaida na mara zote tabia yake imekuwa ni ya kupendeza.

Kwetu vijana wa Tanzania, tupambane na changamoto zetu tukiwa na nguvu ya kufikia malengo yetu bila kutafuta sababu za kushindwa.

Francis Daudi,
Kijana Mwenzenu.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com