Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,
Angellah Kairuki amesema watumishi wa umma walioghushi vyeti
watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Kairuki
amesema hayo jana (Julai 11) katika kikao kazi na watumishi na
viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, Tarafa ya Mbagala.
Alisema wote walioghushi vyeti hawapo kazini na wameshafutwa katika orodha ya malipo ya Serikali.
Waziri
alielekeza waajiri kuwafuta wote wasiostahili kuwepo katika orodha ya
malipo na wasimsubiri hadi afike katika maeneo yao ya kazi ili
kutekeleza agizo hilo.
“Baada
ya uhakiki kukamilika, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa walioghushi
vyeti kwa kuzingatia sheria, kanuni, utaratibu na miongozo iliyopo
katika utumishi wa umma,” alisema Kairuki kama alivyokaririwa katika
taarifa iliyotolewa na wizara.
Aliwataka
waajiri kuhakikisha wanahakiki taarifa za watumishi wapya wanapoajiriwa
na wale wanaohamia ili kujiridhisha kama wana vyeti safi.
“Ni
wajibu wa kila mwajiri kuhakikisha kuwa vyeti vya kila mwajiriwa mpya
vinathibitishwa na mamlaka husika kabla ya kumwajiri na hatimaye
kumuingiza kwenye orodha za malipo ya mshahara kupitia mfumo wa HCMIS na
mifumo mingine ya mishahara ya kitaasisi,” alisema.
Akizungumzia
watumishi wa umma walioajiriwa na sifa za darasa la saba, Kairuki
alisema endapo aliajiriwa kabla ya Mei 20 mwaka 2004 anastahili
kuendelea kuwa katika utumishi wa umma na endapo kajiendeleza
abadilishiwe muundo kuendana na sifa za elimu aliyopata.
Alisema endapo mtumishi huyo aliajiriwa baada ya Mei 20 mwaka 2004 anatakiwa kuwa na sifa ya elimu ya kidato cha nne.
Kairuki
pia alitoa ufafanuzi wa kazi inayoendelea inayohusu kuoanisha taarifa
za watumishi na zile za usajili uliofanywa na Mamlaka ya Vitambulisho
vya Taifa (Nida).
“Uhakiki
huu utaongeza usahihi wa taarifa za watumishi nchini, kudhibiti
watumishi hewa, udanganyifu wa taarifa zinazomhusu mtumishi na
kutekeleza azma ya Serikali ya kuunganisha mifumo ya kimkakati ya Tehama
ili ibadilishane taarifa,” alisema.
Katibu Tawala Mkoa wa Dar e Salaam, Theresia Mbando alimpongeza Waziri Kairuki kwa kuboresha utumishi wa umma.
Mbando
alisema sasa watumishi wa umma waliobaki kazini wameweza kuziba pengo
la waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi na kuondolewa kazini.
0 comments:
Post a Comment