METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, July 17, 2017

UVCCM ZANZIBAR YATAKA WIZARA YA ELIMU SMZ IJITATHMINI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu Waandishi wa habari kwanza kabisa napenda kumshuru Mwenyezi Mungu mtukufu muumba ardhi na Mbingu na vyote vinavyoonekana na visivyo onekana kwa uwezo wake wa kutajaalia uhai na uzima tukaweza kukutana leo hii.

Poleni na majukumu mazito ya kila siku na hongereni kwa kuendelea kuuhabarisha umma habari mbali mbali zinazotokea kwenye jamii inayowazungaka huku mkitumia vyema taaluma yenu ya habari kwa kuzingatia miiko na maadili ya kazi yenu.  

Ndugu waandishi wa habari

Hivi karibuni baraza la mitihani la taifa (NECTA) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato sita kwa mwaka 2017, naamini nyote mmeshayapata au kuyasikia matokeo hayo yanayoonyesha shule kumi zilizofanya vibaya zaidi saba miongoni mwazo ni kutoka Unguja Zanzibar huku katika zile kumi zilizofanya vizuri zaidi hakuna hata moja kutokea Zanzibar.

Umoja wa Vijana wa CCM ZNZ hatukuridhishwa na hatujafurahishwa hata kidogo na matokeo hayo ambayo dhahiri yanaonyesha kuporomoka kwa ufaulu wa vijana katika mitihani ya kitaifa huku matokeo haya mabaya yakielekea kuwa jambo la kawaida kwa skuli zetu.

Kama mtakumbuka hata mwaka uliopita 2016 skuli sita za Zanzibar zilikuwemo kwenye orodha ya skuli kumi zilizofanya vibaya zaidi jambo ambalo miaka ya nyuma halikuwa likitokea.

Ikikumbukwe kuwa skuli zote saba ambazo zimo kwenye orodha ya skuli zilizofanya vibaya zaidi kwa mwaka 2017 katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita kwa mwaka huu zinatoka Mkoa wa Mjini Magharibi 

Ndugu waandishi wa habari

Umoja wa vijana wa CCM ZNZ Tunaitaka Wizara ya elimu na Mafunzo ya amali ya Zanzibar kujitathimini kama wanawatendea haki wazanzibar katika usimamizi wa elimu haswa elimu ya sekondari.

Katika Miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia serekali ya CCM kwa upande wa Zanzibar inayoongozwa na Mhe. Dr ALI MOHD SHEIN ikitenga fedha nyingi kukarabati na kujenga miundombinu mipya ya elimu mijini na vijijini ili kurahisha na kuweka mazingira mazuri na bora kama ilivyoelekezwa katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015 – 2020 ambapo skuli mpya sizizopungua 9 za ghorofa katika visiwa vya Zanzibar zitajengwa sambamba na upatikanaji wa nyenzo muhimu za kufundishia na walimu wenye uwezo mzuri, lakini licha ya jitihada hizi za kuboresha elimu katika sekta ya miundombinu matokeo ya mwisho ya uwekezaji huu hayaridhishi. 

Kwa masikitiko makubwa unaweza kusema kuwa jambo hii la ufaulu mbaya kwa skuli za Zanzibar sasa linataka kuwa ni mazoea kitendo ambacho kinatutia aibu mbele ya macho ya Watanzania na dunia yenye kupenda maendeleo.

UVCCM Zanzibar tunadhani ni vyema wenzetu wa wizara ya elimu, kuanzia waziri mwenye dhamana na watendaji wakuu,  kukaa chini kutathimini kwa kina juu aibu hii na pia ni vyema wakaenda mbali zaidi hata nawao mwenyewe wakajitathmini na kujipima kama kuna umuhimu wa uwepo wao katika nafasi walizonazo hivi sasa

Ndugu waandishi wa habari

UVCCM Zanzibar tunaishauri serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kwa haraka kuunda tume maalum itakayo lichunguza kwa undani suala la kuporomoka kwa ufaulu wa mitihani ya kitaifa na skuli zetu kuwa mkiani na kuja majibu na mikakati madhubuti ya kuondoa kadhia hii miaka ijayo.

Tunaitaka serikali katika tume hiyo ijumuishe wadau wote wa elimu Zanzibar bila kuwasahahu vijana waliopo katika maskuli hivi sasa na wale waliohitimu miaka ya nyuma ili Zanzibar ipate ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili. 

Ikumbukwe hili si tatizo la mtu mmoja, zipo kumbukumbu nzuri sana ambapo wakati ukikaa na kufikiria hupati majibu ya wapi tumejikwaa, mfano tumezoea siku za nyuma kusikia Skuli kama ya LUMUMBA ikitoa wasomi wakubwa sana kwa nyanja tofauti ni skuli ambayo imejijengea umaarufu hata nje ya nchi kwa kutoa wataalamu, wanamichezo mahiri na viongozi mbali mbali ambapo hata RAIS wetu kipezi Dr ALI MOHD SHEIN amesoma shule ya LUMUMBA lakini leo hii Lumumba inasomeka kwenye shule zilizofanya vibaya nchini hii ni aibu kwa sekta ya elimu Zanzibar.

Mwisho UVCCM ZNZ tumechoka kuona skuli za Zanzibar zinasomeka kwa wingi katika shule kumi za mwisho kimatokeo katika mitihani ya kitaifa hivyo tunaamini kama serikali itaunda tume kama tulivyopendekeza na wajumbe wa tume wakaja na ripoti nzuri tutakuwa tumetibu tatizo na kuondoa aibu katika sekta ya elimu Zanzibar. 

Tunawaomba Wazazi kukaa chini na ndugu zetu kuwashauri,  kuwaongoza na kuwaeleza ukweli juu ya hatma ya Taifa letu huku wakiwakumbusha umuhimu wa elimu na faida kwa Taifa, kama Wazazi sasa ni wakati muafaka kutekeleza wajibu wao.

Aidha tunawasihi sana ndugu zetu walio masomoni nao wasiharakie maisha kila jambo linawakati wakati wake, kwa sasa kazi yao wao ni kupata elimu ili kuja kulisaidia Taifa baadae, tunawashi kutumia kila aina uwezo wao ili kujiwekea hatma njema na Taifa kwa ujumla.

Ni imani yetu kuwa tukishirikiana pamoja tutaweza kupiga hatua moja katika kukimbia kadhia hii siku zijazo.

Asanteni

Kidumu CHama Cha Mapinduzi

ABDULGHAFAR IDRISSA

KAIMU NAIBU KATIBU MKUU

UVCCM ZANZIBAR 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com