Na Mathias Canal, Sengerema-Mwanza
Umoja Wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa umevishauri vyama vya Upinzani nchini kutosimamisha mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani kinyume Chake watapata aibu kubwa kuliko chaguzi zingine zote zilizopita tangu kuanza uchaguzi wa vyama vingi mwaka 1995.
Umoja huo umesema kuwa kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli ni wazi kuwa watanzania wanaunga mkono juhudi hizo hivyo wameendelea kuwa na Imani naye sambamba na Imani kubwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ushauri huo umetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa Ndg Shaka Hamdu Shaka (MNEC) Julai 26, 2017 Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza Wakati wa ziara ya siku moja alipokuwa akizungumza na Vijana wa Jumuiya ya Chama hicho (UVCCM) pamoja na wanachama wa chama cha Mapinduzi (CCM) katika Mkutano wa ndani uliofanyika katika Ukumbi wa CCM kijijini Nyakutanga, Kata ya Bukokwa.
Katika mkutano huo Shaka amemuagiza Katibu wa Umoja Wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Sengerema kurejea Majina yote ya wagombea kwani amebaini kuwa kuna Kata ambazo zimepitisha wagombea nafasi Mbalimbali Vijana ambao tayari wamevuka umri wa kikanuni wa miaka 30.
"Ninazo taarifa za kutosha juu ya baadhi ya wagombea ambao wamevuka umri wa miaka 30, kuna mgombea amepitishwa kugombea huku ana miaka 41 na mwingine Ana miaka 38 hivyo wanapaswa kutolewa ndani ya siku mbili la sivyo nitachukua Hatua kwenu Viongozi wa Jumuiya ya Vijana" Alisema Shaka
Shaka alisema kuwa katika Chaguzi zote za Chama Viongozi na wanachama kwa ujumla wake wanatakiwa kufuata taratibu na Kanuni za Uchaguzi ili kupata viongozi mahiri na makini katika uimarishaji wa CCM MPYA na Tanzania Mpya.
Alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi CCM Kimepewa dhamana kubwa na Wananchi ya kuwaletea maendeleo hivyo kufanya mikutano ya ndani nchini ni sehemu ya kuangalia namna utekelezaji wa Imani waliyoitoa Wananchi kupitia ilani inavyosimamiwa.
Shaka amewaomba Vijana wanaogombea nafasi Mbalimbali katika uchaguzi huu kutokata tamaa na kutoa ushirikiano Mkubwa kwa madiwani, Wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli ili kutimiza ndoto ya Tanzania ya maendeleo endelevu.
Alisema kuwa pindi wanapopata taarifa ambazo zinaonyesha uvunjifu wa Kanuni za Uchaguzi kwa kupitishwa wahenga kugombea watoe taarifa haraka ili Hatua za kinidhamu ziweze kuchukuliwa.
Katika Ziara hiyo Kaimu Katibu Mkuu huyo ameshiriki ujenzi wa shule ya Sekondari Bukokwa ambayo ujenzi wake umeshirikisha nguvu za Wananchi sambamba na fedha taslimu ili kusaidia kukamilika haraka kwa ujenzi wa shule.
Aidha, Shaka alizindua shina la Wakereketwa UVCCM Kata ya Bukokwa ambapo Ungozi wa shina hilo la Wakereketwa waliomba kupitia Mfuko wa Umoja Wa Vijana wa 5% kupatiwa fedha ili kukamilisha baadhi ya mapungufu waliyonayo katika vikundi vyao vilivyosajiliwa.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment