Tarehe
05 Agosti, 2017 siku ya Jumamosi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe.
Yoweri Kaguta Museveni wataweka jiwe la msingi la Mradi wa bomba la
kusafirisha mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda
hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Mradi
huu ni moja ya miradi mikubwa ambayo nchi yetu imeipata na kuanza
kutekeleza tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani tarehe 05
Novemba, 2015. Ni mradi ambao uwekezaji wake ni mkubwa wa Dola za
Marekani Bilioni 3.5 sawa na takribani Shilingi Trilioni 8 za
kitanzania.
Urefu
wa bomba hili ni kilometa 1,445 na kati ya hizo kilometa 1,115
zinajengwa Tanzania na mafuta ghafi yatakayosafirishwa ni mapipa 216,000
kwa siku.
Inatarajiwa
wakati wa ujenzi wa mradi huu ajira takribani 10,000 zitazalishwa na
Watanzania watakuwa wanufaika wakubwa wa ajira hizi. Nchi zetu za
Tanzania na Uganda zitapata manufaa makubwa ya kiuchumi kutokana na kodi
na tozo mbalimbali, mrahaba na shughuli nyingine za kibiashara
zitakazoambatana na mradi huu.
Nachukua
fursa hii, kuwaalika Watanzania wote kufuatilia matangazo ya moja kwa
moja yatakayorushwa na vituo vya redio, televisheni na mitandao ya
kijamii kwa siku hiyo ya Sherehe za uwekaji jiwe la msingi na pia
kufuatilia matangazo mbalimbali na machapisho yatayotolewa na vyombo
vyetu vya habari na mitandao ya kijamii kuelekea siku hiyo.
Kama
ambavyo viongozi wa Mkoa wa Tanga wanafanya, tunataraji wananchi wa
Tanga watajitokeza kwa wingi kuungana na Rais wao Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli na Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni katika sherehe
hii kubwa na kwa mradi huu mkubwa katika nchi zetu.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
28 Julai, 2017
0 comments:
Post a Comment