“Kama msomi wa Afrika, mzigo mkubwa ulionao ni kuwakomboa waafrika wenzako maskini wasio na elimu, wasio na uwezo na waliogandamizwa na minyororo mikubwa ya umaskini, udhalimu na uzalilishaji mkubwa”. Hayo yalisemwa leo 04/06/2017 na aliyekuwa Mgeni Rasmi katika mahafali ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Kilimanjaro Ndg. Humphrey Polepole Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi alipokuwa akihutubia mamia ya wanachama wakiwemo wahitimu katika ukumbi wa CCM Mkoani Kilimanjaro.
Ndg. Humphrey Polepole alisema, Kila kijana wa Afrika akifahamu kwamba mzigo alioubeba si wake peke yake, atasoma kwa bidii akijituma kabisa sio kwa sababu tu anatafuta cheti bali ni kwa sababu anatafuta MAARIFA na TAARIFA SAHIHI zitakazo muwezesha kupata uelewa wa masuala mbalimbali yanayozunguka katika Taifa lake, bara lake na ulimwengu mzima ili AINUKE akawe MTU RASILIMALI ambaye sio tu wa familia, jamii, nchi, au bara lake bali ulimwengu nzima ukanufaike kwa uwepo wake.
Sisi wote maishani mwetu lazima tuwe na malengo, na katika hayo lazima liwepo LENGO MOJA KUBWA. Lengo ambalo kwa utimilifu wake litakuwa ni TIJA na FURAHA kwa wengi, lengo ambalo kwa utimilifu wake litaibua sala za SHUKRANI kwa watu hata tusiowajua juu ya uwepo wetu duniani.
Akiendelea kutoa ufafanuzi juu ya juhudi zinazofanywa na Mhe. Rais Dr. John Pombe Magufuli na Serikali yote ya Awamu ya Tano dhidi ya kuimarisha Nidhamu na Uchumi wa nchi, Ndg. Humphrey Polepole alisema, Afrika ndilo Bara pekee ambalo lina utajiri wote kwa kiwango cha juu kabisa kuliko mabara mengine yoyote, kwa utambuzi ambao umekwisha kufanyika mpaka sasa hivi. Ukizungumzia Almasi yote duniani takribani asilimia 90 inapatikana na bado ipo katika Ardhi ya Bara la Afrika. Dhahabu yote iliyopatikana duniani zaidi ya asilimia 40 yake ni ile ambayo imetoka katika Bara la Afrika. Ipo haja ya kuungana kwa pamoja kama Taifa ili tuweze tuweze kuukomboa uchumi wetu.
Ndg. Polepole aliendelea "Tupatieni vongozi ambao watajitolea nafsi zao kuondoa maradhi, magonjwa na dhuluma, watashirikiana na wenzao wote kujenga nchi yetu na watakuwa wanachama waaminifu wa Chama Cha Mapinduzi kama ambavyo ahadi zake zinavyojieleza".
Mahafali hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Jumuiya zake wakiwemo Mwenyeviti na makatibu wa Chama wilaya na Mkoa, Uongozi wa Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa, na wanachama wa CCM kutoka matawi mbalimbali ya Vyuo na Vyuo Vikuu yakiwemo KCMC, USHIRIKA (MOCU), MWENGE, SMMUCO Town Compus, SMMUCO MASOKA, SMMUCO MWIKA pamoja na MWEKA ambapo Jumla ya wanachama mia sabini na saba 177 kutoka Matawi ya vyuo mbalimbali walitunukiwa vyeti vya kuhitimu masomo yao.
0 comments:
Post a Comment