METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, June 27, 2017

Umeme wa uhakika wanukia

Rais John Magufuli akiwa na watumishi wa Kitengo cha Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi ambayo ilikuwa chini ya Ofisi ya Rais (PDB) waliokuwa wakisimamia utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Ikulu, Dar es Salaam

RAIS John Magufuli amekutana na timu ya wataalamu wa masuala ya umeme na ujenzi wa miundombinu ya mabwawa ya maji kujadili mradi mkubwa wa kuzalisha umeme mwingi hapa nchini.

Rais alikutana na wataalamu hao na kujadiliana kuhusu utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa uzalishaji wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stiegler’s Gorge Power Project) wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,100 za umeme.

Rais alikutana na wataalamu hao ikiwa ni utekelezaji wa nia yake ya kuhakikisha mradi huo unaanza kujengwa haraka iwezekanavyo na kuzalisha umeme mwingi utakaosaidia kuharakisha maendeleo hapa nchini, hususani ujenzi wa viwanda. “Kesho (leo) Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn anawatuma wataalamu wake waliojenga mradi mkubwa wa bwawa la maji la kuzalisha umeme kule Ethiopia, wakiwa hapa mtakutana nao na mtabadilishana uzoefu, nataka na sisi tusichelewe, tuzalishe umeme utusaidie kwenye ujenzi wa viwanda,” alisisitiza Rais Magufuli.

Wakati huo huo, Rais Magufuli jana alivunja rasmi kitengo kilichokuwa kinasimamia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kilichoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Nne, ili mageuzi katika kusimamia sekta kuu za kitaifa za kipaumbele ili kuharakisha upatikanaji wa huduma kwa umma.

Kitengo hicho cha Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi ambayo ilikuwa chini ya Ofisi ya Rais (PDB) baada ya kuvunjwa, wafanyakazi wake wamehamishiwa katika ofisina taasisi nyingine za Serikali kwa ajili ya kuendelea na utumishi wa umma.

Taarifa iliyotolewa jana Ikulu, ilifafanua kuwa Rais Magufuli aliagana na wafanyakazi hao jana katika hafla iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam akiwashukuru kwa kazi nzuri waliyoifanya wakiwa PDB na kuwataka kuendelea kulitumika taifa kwa juhudi na maarifa wakiwa katika ofisi nyingine walizopangiwa. “Natambua kuwa nyie ni wafanyakazi wazuri wenye ujuzi na maarifa muhimu kwa ajili ya Taifa letu.

Mmetoa mchango mkubwa mlipokuwa PDB nategemea mtaendelea hivyo na hata zaidi katika ofisi mbalimbali mlizopangiwa, mkachape kazi kwa kutanguliza maslahi ya Watanzania,” alisema Rais Magufuli. BRN ni mfumo maalumu wa utekelezaji wa miradi unaotumika kutekeleza Sekta Kuu za Kitaifa za Kipaumbele (NKRAs) ili kuharakisha upatikanaji wa huduma kwa umma ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2025, ya kuifanya Tanzania ifikie hadhi ya nchi yenye uchumi wa kiwango cha kati.

Mfumo wa BRN unajumuisha mkakati wa utekelezaji, muundo wa usimamizi wa utekelezaji katika ngazi ya wizara na mipango mikakati. Kwa pamoja, mikakati hii inajenga mfumo wa maendeleo unaoweka vipaumbele katika ushirikishaji, uwazi na uwajibikaji. BRN ni mfumo ambao uliigwa na Serikali ya Tanzania kutoka Malaysia na utekelezaji wa miradi wa BRN ulianzishwa ili kuleta mageuzi katika utekelezaji wa miradi katika idara na taasisi za Serikali.

Mpango huo ulikuwa unatekelezwa kwa kuweka malengo ya utekelezaji, mfumo madhubuti wa ufuatiliaji wa utekelezaji na nidhamu ya utatuzi wa changamoto zinazojitokeza. Msingi mkuu wa BRN kuweka vipaumbele, nidhamu ya kutekeleza kwa vitendo na uwajibikaji ndivyo vitu vinavyotusaidia kufikia utekelezaji wa haraka wa malengo yetu, kama yalivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya 2025.

Sekta mbalimbali kama Kilimo, Nishati, Uchukuzi, Maji na Utafutaji wa raslimali fedha ni miongoni mwa sekta ambazo ziliwekwa chini ya BRN na Serikali ya awamu ya awamu ya nne. Hata hivyo tangu kuingia madarakani Rais Magufuli, kitengo hicho kilijikuta hakina kazi kutokana na Rais kuja na mfumo mwingine wa ufuatiliaji wa utendaji wa wizara, taasisi na wakala wa serikali. Kutokana na hali hiyo BRN, wakajikuta hawana kazi za kufanya jambo ambalo jana kitengo hicho kimezikwa rasmi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com