Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan
amewataka wananchi kote nchi kuwafichua watu wanaonyanyasa na
kudhalilisha watoto kijinsia ili waweze kukamatwa na kuchukua hatua za
kisheria kama hatua ya kukomesha vitendo hivyo ambayo vimeanza kushamiri
katika baadhi ya jamii nchini.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan
ametoa agizo hilo katika hotuba yake ya kuhitimisha kampeni ya kudhibiti
magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo ilitoa huduma bure za vipimo na
matibabu kwa watoto na vijana zaidi ya 1500 kampeni ambayo iliambatana
na maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika katika viwanja vya Shule ya
msingi Kinyerezi mkoani Dar es Salaam.
Makamu
wa Rais amesema kuwa watenda maovu hao lazima vifichuliwe na wananchi,
walezi pamoja na wazazi kwa kuwa watu wanaofanya vitendo hivyo vya
udhalilishaji wa watoto wapo miongoni mwa jamii.
Katika
kukabiliana na hali hiyo, Makamu wa Rais ameviagiza vyombo vya dola
kutofumbua macho vitendo hivyo bali pindi wanapopata taarifa za matukio
ya udhalilishaji wa watoto wachukue hatua za haraka za kuwakamata na
kuwachukulia hatua stahiki watu wanaofanya vitendo hivyo vibaya.
Makamu
wa Rais pia ametoa wito maalum kwa wanafunzi wa shule za msingi na
sekondari kote nchini waache kuwaficha watu wanaotendea vitendo hivyo
vibaya bali wawapatie taarifa walimu wao na polisi ili wahusika waweze
kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Amesema
kwa kufanya hivyo watoto watakuwa salama katika mazingira ya nyumbani
na wakiwa mashuleni kwani watu wabaya wanaofanya vitendo hivyo
watawajibishwa kulingana na matendo maovu waliyokuwa wanawafanyia watoto
hao.
“Mtoto anaweza kufaidika na fursa sawa iwapo tu atalindwa kwa kuwezeshwa kuwa afya bora”, Amesisitiza Makamu wa Rais.
Kuhusu
kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Makamu wa Rais Mhe Samia
Suluhu Hassan amesema magonjwa yasiyo ya kuambukiza yameendelea kuua
watu kwa kasi katika nchi zinazoendelea Kusini mwa Jangwa la Sahara
ikiwemo Tanzania.
Amesema
ipo haja ya kuimarisha juhudi za kukabiliana na tatizo hilo kwa
ushirikiano wa wadau wote kwani janga hilo linagharimu taifa na wananchi
wake wakiwemo watu wazima, watoto na vijana.
“Magonjwa
yasiyo ya kuambukiza yasipodhibitiwa yatapunguza uzalishaji
mali,ufanisi mahali pa kazi na hata shughuli za ulinzi na usalama nchini
mwetu na hivyo pato la taifa litapungua na taifa kuwa watu maskini
kutokana na magonjwa hayo”, Alifafanua Makamu wa Rais.
Makamu
wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kuwa katika kukabiliana na
magonjwa yasiyo ya kuambukiza Serikali imeweza kupanua maeneo ya kutolea
huduma kwa wagonjwa wa saratani nchini kwa kujenga jengo jipya katika
Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kuongeza majengo mapya ya huduma za
saratani kwenye Hospitali za Rufaa ya kanda ya Bugando mkoani Mwanza.
Amesema
Serikali pia imejenga Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambayo ni
taasisi ya mfano ya kutibu maradhi ya moyo ambapo kutokana na kujengwa
kwa taasisi hiyo Serikali imefanikiwa kuokoa mabilioni ya fedha ambayo
yangetumika kuwagharamia wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dkt Hamisi Kingwangala amemhakikishia Makamu wa Raia kuwa Wizara
hiyo itaendelea kuweka mipango na mikakati imara ya kukabiliana na
magonjwa yasiyo ya kuambukiza nchini.
Dkt
Kingwangala ameomba wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za kidini na
wadau wengine kushirikiana na Wizara ya Afya katika kuongeza kasi ya
kukabiliana na magonjwa hayo ili yasiendelee kuteketeza maisha ya watu
nchini
0 comments:
Post a Comment