METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, June 27, 2017

KKKT wakemea wanaotumia mahubiri kujitajirisha

Na Frank Leonard, Iringa

MKUU wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wamekemea aina ya mahubiri ya dini yaliyochipuka miaka ya karibuni waliyodai yanalenga kuwanufaisha baadhi ya watumishi wa Mungu wanaojiita manabii.

Viongozi hao waliwazungumzia manabii hao (hawakutajwa majina) hivi karibuni mjini Iringa kwenye ibada ya kuwekwa wakfu na kuingizwa kazini Askofu mpya wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Blaston Gaville.

Akitoa nasaha kwa Askofu Gaville, Askofu mstaafu wa KKKT Dayosisi ya Iringa, Dk Owdenburg Mdegella alisema; “Hubiri Injili ya Yesu Kristo, usihubiri biashara ya kiroho, usihubiri fedha, usihubiri mafanikio na udanganyifu wa aina yoyote ile.”

Askofu Mdegella alisema wahubiri wengi nchini wametumbukia katika udanganyifu na kufanya mahubiri kama vyama (Saccos) vya kutajirisha watu. “Kazi ya maaskofu na viongozi wa makanisa ni kuhubiri Injili na Kanisa na kuwa msemaji wa watu kwa Kaisari na msemaji wa Kaisari kwa watu,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kasesela alisema makanisa yanakabiliwa na changamoto kubwa kwani viongozi wake wamekuwa watu wa kujinufaisha. “Suala la fedha linatiliwa mkazo kuliko Injili, kujinufaisha huko kumepitiliza hadi kwenye kwaya, kuna baadhi ya waimbaji huwezi kupata huduma yao bila kulipa mamilioni, imekuwa biashara wakati Mungu alikataa kufanya biashara kanisani,” alisema.

Kasesela ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Ushauri ya KKKT Taifa, alitaja changamoto nyingine zinazoyakabili baadhi ya makanisa kuwa ni unabii wa uongo unaofanywa kwa kuwatumia watu wanaodanganya kuponywa kutoka kwenye matatizo yao. “Tunaomba viongozi wa kweli wa makanisa, waendelee kutuombea ili kuwanusuru watu wenye kiu ya Neno la kweli la Mungu wasiendelee kupotea,” alisema.

Naye Askofu Mkuu wa KKKT, Dk Fredrick Shoo alisema; “Tupo katika kipindi ambacho baadhi ya viongozi wa dini wanawarudisha watu katika hofu na woga waliokuwa nao kabla Yesu Kristo hajatuweka huru.”

Aliwataka Watanzania kujihadhari na matapeli wanaojiita manabii au watumishi wa Mungu ambao nia yao ni kutumia udhaifu wa mwanadamu kujitajrisha. “Wapo watu wanafanyiwa mambo mabaya sana, wanafilisiwa au kupotezewa mali zao na ndoa zao zinavunjika kwa sababu ya hawa manabii wadanganyifu na wenye hila chafu za kishetani,” alisema.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com